Monday, July 19, 2010

MAAZIMIO YA KONGAMANO KUHUSU KURA YA MAONI NA SERIKALI YA UMOJA W AKITAIFA LILILOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA BAYTUL YAMIN ZANZIBAR, TAREHE 17-18 JUL 2010

Sisi Wazanzibari washiriki wa Kongamano kuhusu Kura ya Maoni na Serikali ya Umoja wa Kitaifa lililofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 17-18 Julai 2010:

Tunawapongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na kusahau siasa za chuki na uhasama baina ya vyama vyao viwili;

Tunaamini viongozi hao wawili wataingia katika vitabu vya historia na kukumbukwa milele na vizazi vya Taifa hili, kwamba ni kutokana na ujasiri wao ndipo Zanzibar kwa mara ya kwanza ikaacha kuwa mtumwa wa historia yake ya vurugu za kisiasa na uhasama usiokwisha;

Kwamba kutokana na msimamo wao usiotetereka, Zanzibar ya leo imejenga imani na kuanza kuona mwanga wa matumaini wa Zanzibar ya kesho yenye ustawi, mapenzi na mshikamano, Zanzibar yenye mvuto kwa Wana wa Zanzibar walio ndani na nje ya visiwa hivi vyenye rutba na zawadi kemkem kwetu kutoka kwa Muumba;

Kwamba washiriki wa Kongamano wanawapa hongera waheshimiwa Wawakilishi wote, wakiongozwa na Spika, Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kwa kuungana pamoja kwa ajili ya nchi hii na kusahau tofauti zao za kisiasa katika kusimamia na kuelekeza namna ambavyo Maridhiano ya Viongozi wetu wakuu wa kisiasa yatakavyotekelezwa;

Basi kwa kuzingatia yote hayo sisi Washiriki wa Kongamano hili la Kura ya Maoni na Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Tumeazimia kama ifuatavyo:
1.Tutafanya kila aina ya ushawishi wa halali kuhakikisha kwamba Wazanzibari wanafahamu maana ya Kura ya Maoni na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili wafanye maamuzi sahihi kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar.

2.Tutawashajiisha Wazanzibari kujitokeza kwa wingi na kupiga kura ya NDIO siku ya tarehe 31 Julai 2010 ili kuwezesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuundwa.

3.Kwamba kila Mzanzibari katika nafasi yoyote aliyonayo atumie Uzalendo wake kuwashawishi Wazanzibari wote wachaguwe amani na mshikamano kwa kupiga kura ya NDIO kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

4.Vyombo vya habari vitowe elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa Kura ya Maoni na Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwashajiisha Wazanzibari kupiga kura ya NDIO siku ya Kura ya Maoni.

5.Asasi za kiraia pamoja na jumuiya za kidini lazima zishirikishwe katika mchakato mzima wa Kura ya Maoni na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

6.Tunataraji Tume ya Uchaguzi, ambayo ina mamlaka ya kusimamia Kura ya Maoni, itaheshimu matakwa ya wapiga kura na kutofanya vitendo ambavyo vitaiondolea imani mbele ya macho ya Wazanzibari.

7.Tunawashauri viongozi wote wa kisiasa kuacha ushabiki na utashi wa kisiasa wa kibinafsi na kivyama na kuangalia mustakbal mwema wa Zanzibar.

8.Kwamba Zanzibar hii mpya katu isiwavumilie wote wenye nia ya kutaka kuturudisha katika siasa za chuki na uhasama.

9.Chama cha siasa chochote kitakachopata nafasi ya kuingia katika Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010, lazima kiheshimu maamuzi ya Baraza la Wawakilishi kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hiyo iwe moja katika ahadi zake wakati wa kampeni.

10.Vyombo vyote vya ulinzi vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vya Serikali ya Mapinduzi viwe tayari kuilinda na kuitetea Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa hali yoyote na viache vitendo vya kujihusisha na siasa.

11.Mahkama Kuu ya Zanzibar iwezeshwe kifedha na kiutaalamu ili iweze kuwa ni muhimili mkuu wa demokrasia Zanzibar.

12.Elimu ya uraia (civic education) iendelee kutolewa hata baada ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuundwa ili kuendelea na utulivu na mshikamano wa kisiasa Zanzibar.

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

IMEPITISHWA ZANZIBAR HII LEO TAREHE 18 JULAI 2010.


No comments:

Post a Comment