Sunday, July 18, 2010

DUNIA YAADHIMISHA SIKU YA KUZALIWA KWA MANDELA


Rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela leo anatimiza miaka 92, huku ulimwengu ukisherehekea kwa mara ya kwanza, "Siku ya Nelson Mandela Duniani" kwa heshima ya kiongozi huyo.

Viongozi wa kimataifa na watu wa kawaida nchini Afrika Kusini na nje ya nchi hiyo, wameahidi kujitolea kuhudumia jamii kwa dakika 67 katika ishara za kuadhimisha miaka 67 ya kiongozi huyo kushughulikia harakati za kisiasa.

Mwaka 2009, Umoja wa Mataifa uliamua kuitambua tarehe 18 Julai - siku alizozaliwa mzee Mandela, kama "Siku ya kimataifa ya Nelson Mandela" na itakuwa ikisherehekewa kote duniani. Kwa mujibu wa familia yake, kiasi ya watoto 100 kutoka vijiji vilivyo karibu na kule alikozaliwa, watakuwa nae leo hii.

Tangu kuondoka madarakani, Mandela amejitokeza hadharani mara chache tu. Juma lililopita alikwenda kwenye uwanja wa michezo wa Soccer City mjini Johannesburg, kuwapungia mkono mashabiki wa kandanda kabla ya kufunguliwa mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia, lakini hakubakia kutazama mchezo kwa sababu ya hali yake dhaifu ya afya.

No comments:

Post a Comment