Friday, July 16, 2010

MAHAKAMA YA ICC YAMUACHIA HURU KIONGOZI WA WAASI KONGO

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC yenye makao yake The Hague Uholanzi imeagiza kuachiliwa huru kwa Kiongozi wa zamani wa waasi wa Congo Thomas Lubanga. Mahakama hiyo ilisema hakuna haja ya kuendelea kumzuilia Lubanga, ambaye kesi dhidi yake ilisimamishwa wiki moja iliopita. Lubanga ambaye amekuwa kizuizini kwa miaka minne, alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita.

Thomas Lubanga kiongozi wa zamani wa waasi nchini Congo alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya Uhalifu wa kivita- kwa kuwasajili kwa nguvu watoto waliokuwa chini ya umri wa miaka 15- kujiunga na kundi lake la Union of Congolese Patriots kwa nia moja tu ya kulimaliza kabila hasimu katika vita vya mwaka 1998 hadi 2003 katika Jamhuri ya Kideomkrasia ya Kongo.



Lubanga ambaye kesi yake ilianza kusikizwa Januari mwaka jana- na kugonga vichwa vya habari kwa kuwa ndio ilikuwa kesi ya kwanza mbele ya Mahakama hiyo ya uhalifu huko the Hague Uholanzi- alionekana kupata afueni wiki iliopita, pale kesi dhidi yake iliposimamishwa. Mahakama hiyo ya ICC ilisema imesimamisha kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa waasi kwa sababu upande wa mashtaka ulikataa kuwasilisha taarifa kwa mawakili wa mshtakiwa.

Suala hili la kubadilishana taarifa kati ya upande wa mashtaka na wanasheria wanaomwakilisha Lubanga limeleta utatanishi mkubwa, na lilikuwa sababu ya kucheleweshwa kuanza kwa kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa waasi. Pia kumekuwa na mvutano kuhusu ushahidi uliopo dhidi ya mtuhumiwa huyo.

Hata hivyo Koti hiyo ya uhalifu ilisema agizo la kuachiliwa huru kwa Lubanga halitatekelezwa mara moja, kwa sababu wanataraji upande wa mashtaka utakata rufaa katika siku tano zijaazo. Na naam kabla ya wino wa majaji hao kukauka Kiongozi wa Mashataka wa mahakama hiyo Louis Moreno Ocampo alitangaza atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa kumuachilia huru Lubanga.

Vile vile Mahakama hiyo ilisema kuachiliwa huru kwa Lubanga kunategemea iwapo matayarisho yatakuwa yamekamilika ya kumsafirisha katika nchi ambayo itakuwa tayari kumpokea.

Lubanga amekuwa akizuiliwa tangu Machi mwaka 2006- kwa mashtaka ya uhalifu wa kivita nchini Kongo kwa kuwasajili vijana wadogo na kuwapa mafunzo ya kutekeleza mauaji na visa vingi vya ubakaji. Inasemekana Kiongozi huyo wa zamani wa waasi alikuwa anawasajili watoto wadogo wengine chini ya umri wa miaka kumi kutoka kabila la Hema ili kupigana na kabila hasimu la Lendu.

Wanasheria wanaomuakilisha Lubanga hata hivyo wameshikilia kuwa ushahidi dhidi ya mteja wao ilikuwa hila tupu.


No comments:

Post a Comment