Tuesday, July 20, 2010

CLINTON AZITOLEA WITO SCOTLAND NA UINGEREZA


Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton amezitolea wito serikali za Scottland na Uingereza kupitia upya uamuzi walioutoa mwaka uliopita wa kuachiwa huru kwa mtu pekee aliyehukumiwa kuhusika na shambulio la bomu mwaka 1988 dhidi ya ndege ya Marekani huko Lockerbie, Scottland.

Abdel Baset al-Megrahi, raia wa Libya alihusishwa na shambulio hilo la ndege ya abiria ya Pan Am lililowaua abiria 270. Bibi Clinton aliwaandikia barua maseneta wanne wa Marekani akisema kuwa alizitaka serikali hizo kupitia upya mazingira yaliyosababisha uamuzi huo kufikiwa. Al-Megrahi aliachiwa huru Agosti mwaka 2009 kwa misingi ya huruma kwa sababu alikuwa akiugua saratani ambayo madaktari walisema alikuwa na miezi mitatu tu ya kuishi.

Hata hivyo, bado yuko hai hadi sasa. Suala hilo huenda likajadiliwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na Rais Barack Obama wa Marekani katika mkutano wao wa leo pamoja na suala la kuvuja kwa kisima cha mafuta cha kampuni ya mafuta ya BP na vita nchini Afghanistan.

1 comment:

  1. ndio kesha toka itasaidia nini? na hawana uhakika na uhai wa mtu

    ReplyDelete