Tuesday, July 20, 2010

BAADHI YA TIMU ZINAZOSHIRIKI LIGI KUU UINGEREZA ZAPIGA MARUFUKU VUVUZELA


Timu sita nchini Uingereza ambazo zinashiriki ligi kuu nchini humo zimepiga marufuku kwa mashabiki kuingia katika viwanja vyao huku wakiwa na matarumbeta al-maarufu " vuvuzela".

Timu za Arsenal na Tottenham ndizo timu za mwanzo kupiga marufuku mavuvuzela kuingia katika viwanja vyao huku zikifuatiwa na timu za Liverpool,Sunderland, Birmingham na Westham.

Kwa upande wa timu ya Tottenham wameeleza sababu kuu ya kupiga marufuku vuvuzela ikiwa ni pamoja na usalama uwanjani hapo, wamesema kwamba ikiwa watu watashangiria kwa kutumia vuvuzela kuna uwezekano mkubwa wa watu kushindwa kusikia matangazo yatakayotolewa iwapo itatokezea ajali uwanjani hapo.

Katika sababu zilizotolewa na timu nyengine ni kwamba iwapo wataruhusu ushangiriaji wa vuvuzela wanaweza wakapoteza kawaida na desturi za ushangiriaji katika viwanja vyao.

Vuvuzela zimejipatia umaarufu mkubwa katika fainali za kombe la Dunia huko Afrika Kusini ambapo watu wengi walivutiwa na mtindo wa ushangiriaji kwa kupuliza zumari hizo za plastiki ambapo baadhi ya watu walionesha kukerwa na ushangiriaji kwa kutumia vuvuzela.

No comments:

Post a Comment