Mfuko wa TAifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeanza kuwapatia huduma ya matibabu askari polisi na uhamiaji Zanzibar pamoja na familia zao.
Mkurugenzi wa mfuko huo Kanda ya Mashariki, Rose Ongala, alibainisha hayo juzi wakati wa kukabidhi vifaa yakiwemo mashuka na vifaa kwa wodi za wazazi Kisiwani Unguja na Pemba.
Alisema kwamba tangu kuanzishwa kwa mfuko huo askari polisi na uhamiaji Zanzibar walikuwa hawanufaiki na mfuko huo kwa vile Serikali ya Muungano ilikuwa bado haijawaruhusu kuwa wanachama wa mfuko huo.
“Askari wote wa polisi na uhamiaji wataanza kutibiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuanzia Julai mwaka huu,” alisema mkurugenzi huyo.
Rose alisema kwa upande wa Tanzania Bara pia askari magereza, polisi, zimamoto na Idara ya Uhamiaji wataanza pia kunufaika na mfuko huo.
Alisema kwamba mfuko huo hivi sasa Zanzibar una wanachama 452 pamoja na wategemezi 2,499 wananufaika na mfuko huo.
Aidha, alisema askari hao watakuwa wakichangia asilimia 3 mfuko huo sawa na waajiri wao na watapatiwa matibabu hadi mwisho wa maisha yao.
Alisema tayari kazi ya kuwasajili askari hao Tanzania Bara na Zanzibar imeaanza kufanyika na serikali ya Muungano imeamua kuchukua uamuzi huo, ili kuwaondolea usumbufu wa matibabu askari wake.
Awali akipokea masaada huo kiongozi mwandamizi kutoka Wizara ya afya na Ustawi wa jamii Zanzibar, Septuu Hafidhi Halfan, alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kwa vile utaweza kuwasaidia mama wajawazito na watoto katika hospitali hizo.
***Tz Daima
No comments:
Post a Comment