Saturday, July 3, 2010

AKINA SHEIN, NAHODHA, SHAMHUNA TUMBO JOTO

Na Mwinyi Sadallah

Wagombea 11 wa nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaanza kujadiliwa leo na kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar kabla ya kufanyika uchaguzi wa mwisho Julai 9, mwaka huu mjini Dodoma.

Tayari CCM Zanzibar wametangaza sifa 13 zinazopaswa kuzingatiwa kabla ya kuchaguliwa kuwa mgombea wa urais wa visiwa hivyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar,Vuai Ali Vuai, alisema kikao hicho kitafanyika makao makuu ya CCM Kisiwandui kuanzia saa 3 asubuhi chini ya Mwenyekiti wake, Rais Aman Abeid Karume.

Alisema kwamba ajenda kubwa ya kikao hicho ni kupitia majina ya wagombea na kutoa mapendekezo kabla ya kuwasilisha majina hayo katika kikao cha Kamati Kuu kinachotarajiwa kufanyika Alhamisi wiki ijayo mjini Dodoma.

Aidha alisema kwamba vipimo vitakavyotumika kumpata rais wa Zanzibar kwanza lazima awe na sifa 13 zinazotakiwa na chama kabla ya kuchaguliwa kuwa mgombea urais.

“Mgombea urais wa Zanzibar lazima awe na sifa 13 zilizowekwa na chama bila ya kuwa na sifa hizo hufai kuwa rais wa Zanzibar,” alisema Katibu huyo.

Alizitaja sifa hizo kuwa ni mgombea awe mpenda haki, mtu jasiri katika kupambana na dhuluma na maovu, awe mwenye uwezo na upeo wa kuendeleza na kudumisha amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema sifa nyengine ni mtu mwenye kuona mbali, busara na uwezo wa kufanya mamuzi nyeti, awe anakubalika na wananchi na asiye vumilia uzembe katika kulitumikia taifa.

Alisema sifa nyengine ni awe mtu anayeheshimu misingi ya utawala bora na haki za kibinaadmu na mwenye kuchukia vitendo vya rushwa.

Aidha alisema mgombea huyo awe na sifa ya elimu ya chuo kikuu au inayofanana na kiwango hicho, awe kiongozi muadilifu mwenye hekima na busara, na awe na uwezo wa kuliongoza taifa na asiwe kiongozi mvivu katika kusimamia shughuli za serikali.

“Bahati nzuri wagombea wote walojitokeza tunawafahamu hivyo haitakuwa kazi katika kuwapima uwezo wao kwa kuzingatia sifa 13 zilizowekwa na chama” alisisitiza.

Vuai alisema wagombea wote waliojitokeza wanaendelea na afya nzuri kwa vile hadi jana hakuna taarifa yoyote ya ugonjwa iliyoripotiwa kati ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Alisema kwamba wagombea wote watapewa nafasi ya kujieleza katika kikao hicho, baadae kikao kitatoa alama kwa kila mgombea na kuwasilisha mapendekezo yake katika kikao cha Kamati Kuu ambacho kitakuwa na jukumu la kuteua majina matatu ambayo yatawasilishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM taifa kuchagua jina la mgombea mmoja wa nafasi ya urais wa Zanzibar.

Hata hivyo, alisema kwamba alama watakazopewa wagombea na kikao hicho zitaendelea kubakia siri ya kikao pamoja na mapendekezo yake.

Alisema kwamba waandishi wa habari hawataruhusiwa kuhudhuria kikao hicho na kama kutakuwa na taarifa yoyote ya kutoa kwa waandishi wa habari wataitwa kwa wakati huo.

“Tayari wajumbe wameshaanza kuwasili kwa ajili ya kikao kama kilivyopangwa, isipokuwa ndugu zetu waandishi hamtaruhusiwa katika kikao hicho,” alisema Vuai.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CCM Yussuf Mkamba amesema CCM haijatayarisha mgombea kati ya wanachama 11 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo wakiwemo vigogo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au wale wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na Nipashe alisema kwamba kama CCM ingekuwa tayari imetayarisha mgombea basi kusingekuwa na sababu ya kutoa fomu za kugombea nafasi hiyo.

Alisema kwamba CCM si ya viongozi na mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar atatokana na maamuzi ya vikao na si viongozi wa chama hicho.

“Kama tungekuwa na mgombea tayari tusingetoa fomu za kugombea na mgombea wa nafasi za urais wa Zanzibar atachaguliwa kwa wingi wa kura,” alisema Makamba.

Makamba alisema hayo kufuatia taarifa zilizoenea visiwani Zanzibar kuwa chama hicho tayari kimeshateua mgombea wake wa urais wa Zanzibar na kinachoendelea ni kukamilisha taratibu za vikao.

Tayari Wajumbe wa NEC kutoka Kisiwani Pemba, Unguja na wanaoishi Tanzania Bara wameanza kuwasili tangu juzi Zanzibar wakijitayarisha kuhudhuria kikao hicho.

Hata hivyo, mjadala mkubwa umekuwepo Zanzibar kuhusu kisiwa cha Pemba kutoa mgombea urais baada ya wanachama watatu wa CCM kujitokeza kwa mara ya kwanza kuwania nafasi hiyo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vyingi mwaka 1992.

Wagombea hao ni Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mohamed Aboud, na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo, Hamad Bakari Mshindo.

Hata hivyo, wagombea hao wamekuwa wakipata upinzani mkali kutoka kisiwani Unguja baada ya wanachama wanane kutoka kisiwani humo kujitokeza kuwania nafasi hiyo, akiwemo Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi Mstaafu Dk. Gharib Bilal, Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamhuna, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Haroun Ali Suleiman, aliyekuwa katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi Omar Sheha Mussa, mwana Diplomasia mstaafu Muhamad Yussuf Mshamba na mfanyabiashara maarufu, Mohamed Raza Dharamshi.

Kisiwa cha Unguja tayari kimeshatoa marais sita tangu Zanzibar kujikomboa kwa njia ya mapinduzi kutoka katika utawala wa kisultan.

Iwapo wagombea wenye asili ya Pemba watafikia malengo yao ya kisiasa itakuwa ni mara ya kwanza kwa kisiwa hicho kutoa rais wa Zanzibar.

Imeelezwa kwamba wakati wa chama kimoja Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, alijaribu kuwania nafasi hiyo kabla ya kuangushwa na rais mstaafu marehemu Idrisa Abdull Wakili.

Katika hatua nyingine, CCM imesema marufuku mtu yeyote asiyehusika kuonekana akizugukazuka makao makuu ya CCM wakati kikao hicho kikifanyika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Saleh Ramadhan Ferouz, ni wajumbe tu na watendaji ndio watakaotakiwa katika kikao hicho.

“Hairuhusiwi mtu yeyote asiyehusika na kikao hicho kuwepo katika maeneo ya Ofisi Kuu wakati kikao hicho kinafanyika” alisema Katibu huyo.

Aidha aliwataka wanachama wa CCM Zanzibar kuwa watulivu na kuwaachia wajumbe wa Kamati Maalum wa NEC Zanzibar watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia katiba ya chama hicho. Alisema kikao hicho kimetanguliwa na kikao cha secretarieti ambayo imekutana juzi kuyapitia na kuyaratibu majina ya wagombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar.

Uchaguzi mkuu wa Zanzibar unatarajia kufanyika Oktoba 31 baada ya Rais Amani Abeid Amani, kumaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment