Friday, June 4, 2010

WATURUKI WAOMBOLEZA WALIOPOTEZA MAISHA

Maelfu ya waombolezaji walikusanyika jana katika mazishi ya wanaharakati wa Kituruki waliouwawa wakati wa uvamizi wa majeshi ya Israel dhidi ya mlolongo wa meli za misaada. Rais Abdullah Gul amelihutubia taifa hilo lililokasirishwa kutokana na tukio hilo, kuwa uhusiano na Israel hauwezi tena kuwa wa kawaida.

Majeneza ya wengi wa wale waliouwawa yakifunikwa bendera za Uturuki na Palestina yalipelekwa katika msikiti wa mjini Istanbul wa Fatih kwa kuombewa dua, kabla ya kupelekwa katika maeneo wanakotoka kwa mazishi.

Watu wote tisa waliouwawa, ikiwa ni Waturuki wanane , pamoja na Mmarekani mmoja mwenye asili ya Uturuki, walikuwa katika meli ya Mavi Marmara wakati makomandoo wa Israel walipovamia meli yao katika eneo la maji la kimataifa.

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Uturuki vimesema kuwa askofu mmoja wa kanisa Katoliki amekutwa amekufa kwa kupigwa visu leo kusini mwa Uturuki na dereva wake amekamatwa kwa madai ya kuhusika na mauaji hayo. Askofu Luigi Padovese , alikutwa amekufa katika nyumba yake ya mapumziko katika mji wa Iskendrun katika jimbo la Hatay katika pwani ya barahani ya Meditteranean nchini Uturuki. Jimbo la Hatay, linaishi jamii ya waumini wa Kikristo ambao wameishi katika eneo hilo tangu enzi za himaya ya Warumi.

No comments:

Post a Comment