Sunday, June 27, 2010

WATU 16 WAKAMATWA SOMALILAND

Polisi katika jimbo lililojitenga la Somalia, Somaliland, wamewakamata watu 16 kwa madai ya kuhusika na vitendo vya kigaidi, huku raia katika jimbo hilo wakijitayarisha kupiga kura katika uchaguzi wa rais.

Kulingana na vyanzo vya habari maafisa wa usalama waliwakamata washukiwa hao wa kundi la Al-Shabab baada ya kufanya msako, katika hoteli mbili katika mji mkuu wa Somaliland, Hargeisa.

Maafisa wa usalama walihofia kuwa washukiwa hao walikuwa na nia ya kuvuruga uchaguzi huo,.

Rais wa sasa Dahir Rayale Kahin anayepigania muhula wa pili anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kiongozi wa upinzani Ahmed Mahamoud Silanyo.

Uchaguzi huo wa rais unafanyika baada ya kuahirishwa mara tatu, tangu Aprili 2008. Somaliland ilijitangazia uhuru wake kutoka, Somalia mwaka wa 1991, wakati nchi hiyo ilipotumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Tangu hapo Somaliland imekuwa na utulivu, ingawa hakuna nchi yeyote inautambua uhuru wa Somaliland.
.

No comments:

Post a Comment