Saturday, June 26, 2010

MTOTO WA SALMIN AMOUR AAHIRISHA KUGOMBEA ZANZIBAR

Mtoto wa Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Salmin Amour aitwaye Amini, ametangaza kujiondoa kugombea nafasi ya uwakilishi katika jimbo la Magogoni, visiwani humo.

Kadhalika, Amini amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuchukua tahadhari kubwa ikiwemo kuhakikisha mgombea wa nafasi ya urais visiwani Zanzibar anatokana na mapenzi ya Wazanzibar wenyewe na sio mizengwe ama utashi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC).

Alitangaza hatua hiyo jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Nipashe ambapo alisema uwakilishi sio sehemu ya kujifunzia "bembea".

Alisema vijana wengi wamejitokeza kama utitiri kugombea nafasi hiyo huku wengi wao wakiwa hawajui historia ya Zanzibar na ya kwao wenyewe.

Salmin mwenye umri wa miaka 37 alitangaza nia ya kugombea nafasi hiyo ya uwakilishi mapema mwaka huu lakini amesema ameahirisha nia hiyo.

“Kwa sasa ninakwenda kusoma. Miaka mitano ijayo itanikuta nimesharudi, nitagombea inshallah,” alisema.

Aliliambia Nipashe kuwa wakati anatangaza nia ya kugombea, alishauriana na Baba yake, Dk. Salmin Amour ‘Komandoo’aliyekuwa Rais wa Zanzibar kati ya mwaka 1990 hadi 2000.

Alisema hata wakati wa kujiondoa pia alipata ushauri kutoka kwa watu wake wa karibu ambapo alikubaliana nao.

Kwa upande wa mchakato wa kugombea urais visiwani humo. Amini alimuomba Rais Kikwete na wajumbe wa NEC kuhakikisha wanawapatia Wazanzibar mtu wanayemtaka.

Alisema ingawa Zanzibar ina wajumbre 80 wanaoingia katika kikao cha NEC ambacho hufanyika mkoani Dodoma kwa ajili ya kupitisha jina la mgombea urais visiwani humo, lakini uchache wao usiwafanye Wazanzibar wachaguliwe mtu wasiomtaka.

Alikiri kwamba mwaka huu hali ya kisiasa Zanzibar, hususani ndani ya CCM ni ngumu kuliko watu wanavyofikiria na kwamba Rais Kikwete kama mwenyekiti wa chama tawala anatakiwa kutumia busara zake.

"Ili kuweka mambo vizuri ni lazima Wazanzibari wapatiwe mtu anayekubalika na wanachama wa CCM pamoja na wale wa vyama vingine vya upinzani," alisema.

Amini Salmin Amour alisema kama CCM kitatumia utaratibu wa zamani wa kumpitisha mgombea anayetakiwa na NEC watakuwa na wakati mgumu katika kumnadi kwa kuwa atakuwa sio chaguo la watu wa Zanzibar.

"Apitishwe mtu ambaye ana mvuto kwa CCM na upinzani… Wazanzibar wanamjua mgombea wao wanayemhitaji na wanachosubiria ni muda ufike ili wamchague," alisema.

Alisisitiza kwamba CCM visiwani humo hakina hamasa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kutokana na kuwepo kwa mpasuko, hatua ambayo alisema imesababisha wanachama wake kugawanyika na kusema kwamba tatizo lipo ngazi za juu.

Alikiri kuwa mwaka huu wagombea wa nafasi ya urais pamoja na ile ya uwakilishi wamekuwa wengi kupita kiasi tofauti na miaka mingine iliyopita.

Kuhusu vitendo vya rushwa alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imefanya kazi nzuri lakini bado haijaweza kudhibiti hali hiyo.

Alidai bado wanachama na wajumbe wa NEC visiwani humo wanaendelea kufuatwa na kurubuniwa kwa kuahidiwa fedha ili wawaunge mkono baadhi ya wagombea.

No comments:

Post a Comment