Sunday, June 27, 2010

MJAMZITO AISHI KWENYE KALAVATI

Ama kweli duniani kuna mambo, kwani mwanamke raia wa Kenya, Saida Kimuna (39), ameweka makazi ndani ya kalavati la kupitisha majitaka katika barabara ya Boma, mjini hapa kutokana na sababu zisizofahamika, imegundulika.

Mwanamke huyo anayejitambulisha kutoka Kisii, Kenya, amegunduliwa na wananchi wa mtaa wa Liti Kilimo, akiwa ndani ya kalavati aliloligeuza makazi yake ya kulala usiku kwa muda mrefu sasa.

Akizungumza juzi katika eneo la makazi ya mwanamke huyo, Balozi wa Mtaa wa RDD, Samwel Mpeka, alisema baada ya kupata taarifa ya kuwapo mwanamke aliyeweka makazi ndani ya kalavati hilo, waliwasilisha taarifa Polisi.

Hata hivyo, alisema baada ya polisi kuarifiwa mkasa huo, walimchukua na kumpeleka hospitali ya mkoa ili kufanyiwa uchunguzi ikiwamo na kupimwa akili.

“Tuliwaarifu polisi juu ya jambo hilo na walimchukua na hadi hospitali ya mkoa…lakini baadaye mwezi mmoja uliopita, alirudi kuendelea kulala ndani ya kalavati hili,” alisema Mpeka.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Liti Kilimo, Bashir Mambo, alisema viongozi wa mtaa huo wameshindwa kufahamu kilichomrudisha mwanamke huyo hapo.

“Sisi hatujui kama ametoroka wodini … tumemwona tena akiishi ndani ya kalavati hili … jambo ambalo ni la hatari hasa wakati wa usiku,“ alisema Mambo.

Yeye alipohojiwa kuhusu maisha yake ndani ya kalavati hilo, alidai alifika mjini hapa siku nyingi akiwa na lengo la kumfuata shangazi yake, Mary Kiluo.

Hata hivyo, alisema: “Nimetoka Kisii, Kenya … nina wiki mbili sasa nalala ndani ya kalavati, kwa sababu sina ndugu,” alisema mwanamke huyo ambaye alionekana kuwa na ujauzito, naye alipoulizwa alikiri akisema: “ndiyo nina mtoto ndani”.

Kitendo cha mwanamke huyo kuishi hivyo, kuliwashangaza watu wengi walioshindwa kupata majibu sahihi iwapo Mkenya huyo ana matatizo ya akili au la.
.

No comments:

Post a Comment