Baraza la Habari la Kiislam Tanzania (BAHAKITA) limewahamasisha Waislamu nchini kutokipigia kura Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na kuwadanganya kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Msikiti wa Kisumo ulioko Magomeni, Dar es Salaam, Katibu wa Baraza hilo, Sheikh Said Mwaipopo, alisema kutokana na CCM kuwafanyia utapeli wa kisiasa, watazunguka nchi nzima kuhakikisha CCM haichaguliwi katika uchaguzi wa mwaka huu.
“Huu ni utapeli wa kisiasa na ni unafiki na kwa mujibu wa dini yetu, Mtume anatuambia alama za mnafiki ni tatu: moja, akiahidi hatimizi; pili, akisema anasema uongo; na mwisho akiaminiwa haaminiki.
“Haya yote CCM wanayo na yamejionyesha, sisi kama Waislamu hatukuwatuma kuweka suala la Mahakama ya Kadhi ndani ya Ilani yao,” alisema Mwipopo.
Aidha, alisema kwa kushirikiana na baadhi ya wahadhiri wa Kiislaamu Julai 2 wanatarajia kufanya maandamano ya kulaani kitendo hicho cha CCM.
Alisema maandamano hayo yataanzia viwanja vya Mnazi Mmoja na kuishia kiwanja cha Kidongo Chekundu na baadaye kufanyika nchi mzima kwa lengo la kuwashawishi Waislamu kukikataa chama hicho.
Alisema wamelazimika kufikia hatua hiyo kutokana na kadhia iliyotokea iliyosababishwa na matamshi ya viongozi wa CCM akiwemo Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Pius Msekwa, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe.
Katibu huyo alisema CCM imeshindwa kutekeleza ahadi zake kwa Waislamu, hivyo inaonyesha wazi kuwa chama hicho kiliwadanganya Waislamu kwa kuliweka suala hilo katika ilani ya uchaguzi wa mwaka 2005.
Alieleza kuwa Katiba ya nchi inaeleza kuwa serikali haina dini, lakini kwa sasa chama hiki kinaonyesha kinawachonganisha Watanzania na kurukia masuala ya dini katika kufanya kampeni za kisiasa.
Alisema suala la Mahakama ya Kadhi ni suala la Kikatiba, hivyo haihusiani na masuala ya kisiasa na kwamba mwaka 2005 CCM ilifanya utapeli, ili iweze kupita kwa kuahidi kuingiza Mahakama ya Kadhi.
Katibu huyo alisema kutokana na hilo wamejipanga na fedha wanazo, hivyo watazunguka nchi nzima kufanya mikutano ya hadhara na hata misikitini ili mradi wanachama wa CCM waliokuwa Waislamu wahakikishe kuwa wanarudisha kadi hizo na kujiunga na vyama vingine.
“Sisi hatujatumwa kisiasa lakini naamini kampeni zitakazofanyika hata kama wakikataza tutapambana kuhakikisha kuwa CCM inang’oka madarakani kwani si chama hicho tu kuna vyama vingine vingi ambavyo vinaweza kuwatimizia mahitaji yao Waislamu,” alisema Mwaipopo.
Naye Kiongozi wa Khid Mat Dawat Islamia, Alhaji Abubakar Kabunda kutoka Kanda ya Ziwa, alisema tangu awali walieleza kutokuwa na imani na Kamati ya Mufti Issa Shaaban Simba juu ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.
“Tangu awali hatukuwa na imani nayo kwa kuwa hata suala hili limeondolewa kihuni na kwa dharau, lakini hakuna kiongozi yeyote wa BAKWATA aliyewahi kulizungumzia suala hilo; wote wamekuwa kimya kutokana na kufumbwa mdomo kwa kupewa ‘kitu kidogo’,” alisema Alhaji Kabunda.
.
No comments:
Post a Comment