Tuesday, June 29, 2010

DR SHEIN, NAHODHA WARUDISHA FOMU

Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, ni miongoni mwa wanachama waliorejesha fomu ya kuomba kuchaguliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wa kiti cha urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Wana CCM wengine waliorudisha fomu jana ni pamoja na Kamishna mstaafu wa Utamaduni, Hamadi Bakar Mshindo, Balozi Ali Karume na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud.

Nahodha alirejesha fomu yake Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui baada ya kukamilisha kazi ya wanachama wa CCM waliomdhamini katika mikoa mitatu, mmoja kati ya hiyo ukiwa wa Pemba.

Baada ya kukamilisha kwa kazi hiyo, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu na Hamashauri Kuu ya Taifa ya CCM, aliwashukuru wanachama waliomdhamini akiamini kuwa imani walioionesha kwao, bila shaka inampa matumaini mazuri katika safari yake.

“Ninawashukuru sana wanachama wenzangu wa CCM, tumekwenda Pemba na Unguja wamenipa ushirikiano mkubwa sana…Ninawahakikishia sitawaangusha,” alisema Nahodha (48) na kuongeza:

“Kama nilivyosema siku ya Jumatatu, sikuchukua fomu kwa kutania, nimejiandaa vya kutosha.”

Mapema wiki hii, Waziri Kiongozi alikuwa mtu wa kwanza kuchukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar, ambako katika mkutano wake na wanahabari alieleza masuala kadhaa ya kuinyanyua hali ya uchumi kwa wananchi.

Dk. Shein aliwashukuru wanachama wa CCM wa mikoa mitano ya Unguja na Pemba kwa kumdhamini bila ya matatizo katika maeneo mbalimbali aliyotembelea.

“Nawashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi walionidhamini katika mikoa yote mitano ya Unguja na Pemba....tupo katika mchakato na nikimaliza basi nitawashukuru wote wale,” alisema Dk. Shein ambaye kama Nahodha, ni Mjumbe wa Kamati Kuu pamoja na NEC.

Kazi ya urejeshaji wa fomu kwa wagombea mbalimbali wanaowania nafasi ya urais wa Zanzibar, iliratibiwa na Katibu wa Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar, Idara ya Organizesheni, Asha Abdalla Juma.
.

No comments:

Post a Comment