Monday, June 28, 2010

NAHODHA, KARUME KURUDISHA FOMU LEO

Wanachama wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya urais Zanzibar, akiwemo Waziri Kiongozi, leo wanatarajiwa kurejesha fomu.

Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Vuai Ali Vuai amesema, hadi sasa waliothibitisha kurudisha fomu hizo ni Hamad Bakari Mshindo (61), Ali Abeid Karume (60), Mohamed Aboud Mohamed (50) na Shamsi Vuai Nahodha (48).

“Wanachama hao watarudisha fomu saa 6 mchana (Mshindo), saa 9 alasiri (Karume), saa 10.30 jioni (Aboud) na saa 11 jioni atarejesha Nahodha,” amesema Vuai.

Naibu Waziri Kiongozi ambaye ni Waziri wa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna (66), amesema atarejesha fomu leo.

Kwa mujibu wa Vuai, kila mgombea ametakiwa fomu yake iwe na wadhamini 250 kutoka Zanzibar.

Baada ya kurejeshwa, fomu hizo zitapitiwa na Kamati Maalumu ya NEC Jumamosi na baadaye majina kuwasilishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu cha Julai 6, mwaka huu kabla ya maamuzi ya mwisho ya kumteua mgombea mmoja yatakayofanywa na NEC mjini Dodoma Julai 9, mwaka huu.

Dk. Mohamed Gharib Bilal (65), ni mgombea wa kwanza kurejesha fomu, aliirejesha juzi. Hii ni mara ya tatu anagombea nafasi hiyo.

CCM imepanga kati ya Juni 23 na Julai mosi kwa wanachama wake kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya urais kwa Tanzania Zanzibar na Tanzania.

No comments:

Post a Comment