Kamati ya Maandalizi ya Ndani ya Fainali za Kombe la Dunia zilizoanza kutimua vumbi Juni 11 nchini hapa, imesema inafikiria uwezekano wa kupiga marufuku upulizaji wa Vuvuzela ndani ya viwanja kunakofanywa na mashabiki wa soka.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Danny Jordaan, hatua hiyo inaweza kuchukuliwa na kamati yake kutokana na malalamiko yanayotolewa na watangazaji na baadhi ya mashabiki wa nje ya Afrika Kusini.
Vuvuzela mfano wa filimbi ndefu kama tarumbeta, zimekuwa zikitumiwa na mashabiki wengi hasa wenyeji wa timu ya Bafana Bafana ambao hupuliza mfululizo kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mechi kiasi cha kuwa kero.
Vuvuzela zilishawahi kupigiwa kelele hata kabla ya kuanza kwa fainali hizo, lakini Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), likajadili suala hilo na kutupilia mbali malalamiko hayo kwa hoja kuwa kelele hizo zingeongeza mvuto wa fainali hizo.
Akizungumza na Kipindi cha Michezo cha BBC juzi, Jordan alisema kama malalamiko hayo yatazidi, kamati yake itachukua hatua ya kupiga marufuku.
Mbali ya watangazaji na baadhi ya mashabiki kulalamikia kelele hizo, pia hata nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Patrice Evra, amelalamikia kero ya kelele za Vuvuzela ambazo kutokana na wingi wake, kelele zake zinafanana na mzizimo wa nyuki kwenye mzinga.
Kauli ya Evra imekuja baada mechi yao ya ufunguzi iliyopigwa Juni 11 dhidi ya Uruguay ambayo iliisha kwa sare ya bila kufunguna ikitanguliwa na mechi kati ya wenyeji Afrika Kusini na Mexico ambazo zilitoka sare ya bao 1-1.
Wanaopinga upigaji wa Vuvuzela, hawaishii kero ya uwanjani tu, bali kitendo cha mashabiki kupuliza vifaa hivyo hata usiku wa manane kiasi ambacho kinawafanya wakose hata usingizi.
“Ndani ya uwanja kunakuwa na mvumo wa ajabu, kiasi cha kukosa utulivu wakati wote wa mechi, heri mashabiki hao wangekuwa wakiimba nyimbo za kawaida kwa mdomo.”
No comments:
Post a Comment