Awaambia Wazanzibari wakimtuma atatumika
Mgombea anayewania uteuzi wa kiti cha urais visiwani Zanzibar, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amekuwa wa kwanza kurejesha fomu yake huku akisema kwamba safari hii atapambana hadi dakika ya mwisho.
Dk. Bilal ambaye ni mara yake ya tatu kuwania uteuzi wa kiti hicho kinachoshikiliwa na Rais Aman Abeid Karume, alirejesha fomu jana majira ya saa nne katika ofisi ya Makao Makuu ya CCM Kisiwandui kwa mbwembwe, huku akisindikizwa na umati mkubwa wa mashabiki wake.
Wakati akirejesha fomu, Dk. Bilal ambaye ni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), aliongozana na wake zake wawili.
Alisindikizwa pia na baadhi ya wazee wenye ushawishi wa siasa za Zanzibar, huku wengine wakimsubiri kandokando ya barabara kutoka katika ofisi hizo za Makao Makuu ya CCM, hadi katika tawi la wakereketwa la Kisonge, eneo la Michenzani.
Pia alisindikizwa na vijana waliokuwa kwenye msafara wa pikipiki zilizopambwa kwa bendera za CCM pamoja na vikundi mbalimbali vya burudani.
Akizungumza na wafuasi hao wa CCM waliokuwa wamevalia sare za chama chao, Dk. Bilal alisema kuwa kazi waliyomtuma ya kuchukua fomu na kurejesha, ameimaliza na kuwataka mashabiki wake kuwa na subira.
“Ndugu zangu, nawashukuru kwa michango yenu ya fedha za kuchukulia fomu, kazi mliyonipa nimefanya vizuri, tusubiri taratibu zingine zitakazoendelea ndani ya chama Inshallaah Mwenyezi Mungu atatusaidia, Amen,” alisema Dk. Bila huku akishangiliwa na mashabiki wake.
“Napenda kuwaeleza kwamba sikupata shida ya kutafuta wadhamini na nawaomba wote mnaoniunga mkono, mzidi kuomba Mungu mchakato umalizike salama na tukibahatika tutakwenda NEC. Mmenisubiri kwa muda wa miaka kumi, tumebakiza siku chache, nawasihi muwe wavumilivu,” alisisitiza Dk. Bilal.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwake Mazizini, alipoulizwa atachukua hatua gani endapo CCM haitamteua kuwania kiti hicho, Dk. Bilal alisema safari hii atahakikisha anapambana hadi dakika ya mwisho kwa kuwa ridhaa ya kugombea nafasi hiyo kwa mara ya tatu imetoka kwa wananchi.
Akijibu swali kwamba atakubali matokeo kama atashindwa kwa haki, Dk. Bilal alisema yuko tayari kukubaliana na matokeo ya aina yoyote ile kama atashindwa kwenye kura za maoni.
Alipoulizwa kama kuna ahadi yoyote alipewa wakati alipowania kiti hicho mwaka 2005 na baadaye kushinikizwa kuondoa jina lake ili kumpisha Rais Aman Abeid Karume, Dk. Bilal alisema hakuna ahadi iliyotolewa pamoja na kwamba alijitoa kwa maandishi.
Alisema mwaka 2005 alipogombea urais wa Zanzibar, baadhi ya wanachama wenzake walimwona kana kwamba amefanya dhambi kubwa wakati alikuwa sahihi.
“Sikutenda dhambi na hata jina langu lilivyopelekwa kwenye vikao vya juu vya chama, walinisihi sana niondoe jina, nami nilifanya hivyo kwa maandishi lakini hadi leo sijajibiwa hiyo barua yangu, madai kwamba chama kiliniahidi cheo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, hizo ni hisia tu za watu,” alisema Dk. Bilal.
Hata hivyo alipoulizwa ni mambo gani atayafanya endapo atapatiwa ridhaa ya kuwaongoza Wazanzibari, Dk. Bilal alisema anategemea kufanya mabadiliko makubwa na kutekeleza yatakayoachwa na kiongozi aliyetangulia kwa mujibu wa ilani ya chama chake.
Alisema Zanzibar haina msisimko katika masuala ya maendeleo na kukuza uchumi, endapo ataingia madarakani, alisema, atahakikisha anavibadilisha visiwa hivyo ili viweze kwenda sambamba na nchi nyingine ambazo zimo katika Jumuia ya Afrika Mashariki.
Baadhi ya wazee wa Zanzibar ambao wamepata kushika nyadhifa serikalini, Abdul Razak Mussa (Kwacha), Hamidi Amiri Ally na Ibrahim Aman Ibrahimu, walisema kwa nyakati tofauti kuwa ndiyo waliomtuma Dk. Bilal kuchukua fomu kwani safari hii, ndiyo chaguo lao.
Wazee hao walitaka viongozi wa juu wa CCM, kusikiliza matakwa na si kufanya maamuzi yao kama walivyozoea katika miaka mingine ya kipindi cha kumtafuta mgombea urais kwa tiketi hiyo.
“Vikao vya NEC vinatakiwa kujua kwamba mchujo wa kwanza tunao sisi wazee wa mkoa huu na si vinginevyo,” alisema Abdurazak Musa Simai maarufu kwa jina la Mzee Kwacha.
Mzee Kwacha ambaye aliwahi kushika nyadhifa tofauti za juu katika kipindi cha rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alisema kwa kuwa walishawahi kumpigia kura mara mbili na kushinda katika nafasi hiyo, wanaviomba vikao vya juu vya CCM, safari hii vimpitishe kwani hawataki kuongozwa na mtu mwingine.
“Sijatumwa kuzungumza maneno haya na mtu yeyote…hii ni mara yangu ya kwanza kuzungumza maneno haya, hata nikiwa katika shughuli za chama na serikali…nasema Dk. Bilal sasa apewe nafasi ya kuongoza kwani wananchi ndiyo waliomchangia fedha za fomu,” alisema Mzee Kwacha.
Mbali ya Dk. Bilal, wengine waliochukua fomu kuwania kiti hicho Zanzibar ni pamoja na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Balozi Ali Karume na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna.
Wengine ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano, Dk. Ali Mohammed Shein, Hamad Bakari Mshindo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud Mohamed, Mfanyabiashara Mohamed Darammushi Raza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amari, Harouna Ali Suleiman na Mohamed Yusuf Mshamba.
No comments:
Post a Comment