Saturday, June 26, 2010

DR BILAL AREJESHA FOMU ZA URAIS ZANZIBAR

Mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, Mohammed Raza, amesema ataacha kujishughulisha na biashara ikiwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitampitisha kuwania urais wa Zanzibar na kushinda kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Wakati Raza akitangaza hivyo, mmoja wa waliochukua fomu za kuomba kuwania urais wa Zanzibar, Waziri Kiongozi mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amekuwa wa kwanza kukamilisha kazi ya kutafuta wadhamini na anatarajia kuziwasilisha leo saa 4:30 ofisi za CCM Kisiwandui.

Kwa upande wake, Raza aliyekabidhiwa fomu na Naibu Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, alisema ataacha biashara ili kulinda misingi ya utawala bora, isiyotoa fursa kwa kiongozi kama Rais wa Zanzibar kujihusisha na biashara.

Pia Raza, alisema ikiwa atafanikiwa kuteuliwa na hatimaye kuwa Rais wa Zanzibar, ataunda Baraza la Mawaziri lenye watu waadilifu na wanaoheshimika katika jamii.

Raza alisema akipata nafasi hiyo, vipaumbele vya serikali yake vitakuwa ni kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi wa Zanzibar na kuboresha sekta za viwanda, uvuvi, ukusanyaji wa mapato na kuanzisha mfuko wa mikopo kwa wakulima.

“Maisha bora kwa kila Mzanzibari yanawezekana, tupo Wazanzibari milioni moja, lakini mazao Zanzibar yanaoza kutokana na tatizo la ukosefu wa masoko”, alisema Raza.

Raza aliusifu mfumo wa utoaji fomu za kuomba kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, kwamba hautoi nafasi kwa ukabila, ubaguzi wa rangi ama jinsia. Aliahidi pia kuwa ikiwa atachaguliwa, atawatumikia wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza misingi ya mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo alisema ili kuwa na Muungano imara, kuna haja ya kero zinaoukabili zitatuliwe kwa muda mwafaka, ambapo kwa upande wake, alieleza umuhimu wa kuwashirikisha marais wastaafu katika mchakato wa utatuzi huo.

Naye mgombea wa nafasi hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman, alisema kwamba serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni msingi pekee wa kujenga umoja kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema iwapo CCM itampa ridhaa hiyo na hatimaye kuwa Rais, atahakikisha anafanikisha wazo lililoanzishwa na Rais Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusu kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alieleza kwamba wananchi wa Zanzibar waondoe wasiwasi kuhusu uwezo wake katika masuala ya siasa na utawala, kwa vile ana uzoefu baada ya kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya serikali ya CCM.

Aliahidi kulinda misingi ya Mapinduzi na Muungano, na kuweka kipambele kwa kuimarisha sekta za elimu, uvuvi, kilimo na viwanda ili kuongeza ajira na kipato kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake, mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Mohammed Yussuf, alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atayauza kwa mnada magari ya kifahari yanayotumiwa na mawaziri, ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa serikali.

Alisema kutokana na mazingira ya kijografia ya Zanzibar, mawaziri na watendaji wakuu serikalini wanastahili kutumia gari aina ya RAV4.

Pia aliahidi kuimarisha Muungano wa Tanzania kwa kufanya marekebisho ya Katiba ili kuwa na Muungano wenye maslahi kwa pande zote.

Katika hatua ya Dk Bilal kurejesha fomu, waratibu wa kutafuta wadhamini wake walisema mgombea huyo, anatarajia kurejesha fomu ya kuwania nafasi hiyo leo saa 4:30 za asubuhi.

.

No comments:

Post a Comment