Wednesday, June 2, 2010

ISRAEL KUWAACHIA RAIA WA KIGENI WALIOKAMATWA NDANI YA MELI

Israel imesema itawaachia raia wote wa kigeni, ambao walikamatwa na jeshi la nchi hiyo siku mbili zilizopita katika shambulio la umwagaji damu lililofanywa dhidi ya meli iliyobeba misaada kuelekea Gaza.

Israel imechukua uamuzi huo kutokana na matakwa ya viongozi duniani, ambao pia wametaka kufanyika kwa uchunguzi juu ya shambulio hilo la Jumatatu, ambao ulisababisha vifo vya wanaharakati tisa.

Katika mkutano uliofanyika mjini New York Marekani, wanachama wengi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliilaani Israel na kuitaka nchi hiyo kuondoa vizuizi ilivyoweka Gaza.

Msafara huo mdogo wa meli, ulikuwa umeandaliwa kwa pamoja na kundi linalowaunga mkono Wapalestina pamoja na Shirika la Haki za Binadamu la Uturuki.

Uturuki imesema watu wanne miongoni mwa watu tisa waliouawa, ni raia wake na kuliita tukio hilo kama ugaidi wa kitaifa.

Wakati huohuo Serikali ya Israel imesema imewaachia kutoka gerezani ilikokuwa ikiwashikilia wanaharakati wapatao 50 wa Uturuki waliokuwa katika meli hiyo iliyobeba msaada na kwamba watarudishwa kwao.

No comments:

Post a Comment