Monday, June 7, 2010

6 WAFA 29 WAJERUHIWA KWENYE AJALI ZANZIBAR

Watu 6 wamefariki dunia na wengine 29 kujeruhiwa baada ya gari ya abiria waliyokuwa wakisafiria kuangukiwa na gari la kubebea maji katika ajali iliyotokea jana huko eneo la Koani, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Gari aina ya Tata ililokuwa na namba T 807 AHC ililokuwa limebeba maji ilishindwa kupanda mlima na kuanza kurudi nyuma kwa kasi na kuiangukia gari ya abiria yenye namba za usajili Z 609 AB inayofanya safari zake kati ya Machui na mjini Zanzibar

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Makarani Ahmed, aliviambia vyombo vya habari kuwa, ajali hiyo ilitokea baada ya gari ya kubeba maji kufeli kupanda mlima na kuiangukia daladala iliyokuwa na abiria hao.

Akifafanua tukio hilo alisema kuwa kati ya majeruhi hao, 10 ni wanawake, 4 ni wanaume na 11 ni watoto na kusema wengi wao wamekatika miguu na mikono.

Waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni dereva wa daladala hiyo, Salum Ali Issa (38), Salum Ali Ame (40), Yussuf Abdallah Yussuf (79), Abdallah Maulid Abdallah (6), Shaida Amour Abdallah (27) na Asha Abdallah Saleh (30).

Hata hivyo kamanda huyo alisema dereva wa gari ililosababisha ajali alitoweka mara baada ya ajali hiyo kutokea na juhudi za kumsaka dereva huyo zinaendelea.

Ajali hii ilidaiwa na wakazi wa visiwani humo kuwa ni ajali mbaya ya kwanza kutokea toka mwaka huu uanze na wengi kusikitishwa na tukio hilo.

Makarani alisema majeruhi wa ajali hiyo wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment