Thursday, May 6, 2010

WAZANZIBARI SASA KUPIGA KURA BILA YA POLISI

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Jeshi la Polisi nchini limeamua kuondoa utaratibu wa kuweka askari wenye sare na silaha katika vituo vya wapiga kura ili kuwaondolea mazingira ya hofu wananchi wa Zanzibar kuanzia uchaguzi wa Oktoba 31, mwaka huu.

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Jeshi hilo, Kamishina Msaidizi wa Polisi (SACP) Anyisile Kyoso, wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya polisi katika mkutano uliowashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, jumuiya zisizokuwa za kiserirkali na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kyoso alisema kwamba wakati wa uchaguzi askari wote watawekwa katika kambi maalum baadala ya kuzunguuka katika vituo vya kupigia kura ili kuwaondolea hofu wananchi.

Hata hivyo, alisema kila kituo cha kupigia kura watawekwa askari wasiopungua wawili ambao watakuwa na vifaa vya mawasiliano ya kisasa zikiwemo redio zenye uwezo wa kutuma ujumbe na mazungumzo ya moja kwa moja na vifaa vyenye uwezo wa kutuma ramani ya matukio kupitia mtandao wa kompyuta.

Alisema mawasiliano hayo kutoka katika vituo vya kura yatakuwa yakiunganishwa moja kwa moja na kambi maalum za ulinzi na askari watatumwa katika vituo kama kutatokea viashiria vya vurugu.

“Kuwepo askari wengi katika vituo kunaleta hofu kwa wapiga kura, ndio maana tumeamua kutumia teknolojia mpya na ya kisasa ya ulinzi,” alisema.

Alisema askari wamekuwa wakilalamikiwa kuwa hawatendi haki wakati wa uchaguzi na kuongeza kuwa mfumo huo mpya wa ulinzi utasaidia kuleta ushirikiano kati ya jeshi hilo na wananchi.

Aidha, alisema askari lazima awe mtu wa kujichanganya na watu na sio lazima wavae sare wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.

“Katiba zote za nchi zimesisitiza suala la haki za binaadamu na polisi lazima wafahamu kila mtu ana haki ya kupiga kura, ndio maana tumeweka mazingira mazuri ya kuwaondolea hofu wananchi,” alisema Kyoso.

Naye Ofisa Mwandamizi wa Jeshi hilo kutoka Kitengo cha Operesheni cha Makao makuu Dar es Salaam, Nasser Mwakambonja, alisisitiza masimamo huo kwamba askari hawatakaa mitaani kama ilivyozoeleka badala yake watawekwa katika kambi maalum huku wananchi wakiendelea kupiga kura.

Hata hivyo, alisema Jeshi hilo linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo upungufu wa askari, vitendea kazi pamoja na ufinyu wa bajeti.

Alisema vituo vya wapiga kura vipo 55,000 nchini wakati askari wapo 35,000 na kwamba kwa mujibu wa sheria, kila kituo kinatakiwa kiwe na askari wasiopungua wawili

Mkuu wa Operesheni wa jeshi hilo Zanzibar, Kamishina Msaidizi wa Polisi SACP Hamdani Omar, alisema viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini watumie nafasi zao kutoa elimu kwa wananchi ili kuepusha vitendo vya vurugu wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Alisema Jeshi hilo litahakikisha linafanya kazi karibu na vyombo vya habari ili kuona uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya amani.

Aidha alisema polisi watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi zao bila kupendelea chama chochote cha siasa.

Naye Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Khatib, alisema mpango mpya wa ulinzi wa polisi kutumia teknolojia ya mawasiliano utachangia sana kukuza demokrasia na misingi ya utawala bora Zanzibar.

Aidha, badhi ya viongozi wa vyama walisema sio vibaya kwa askari wa vikosi vya SMZ kushirikishwa katika masuala ya ulinzi wakati wa uchaguzi lakini wafanye kazi chini ya maelekezo ya Jeshi la Polisi.

Walisema askari wa vikosi vya SMZ iwapo watafanyakazi chini ya maelekezo ya Jeshi la Polisi malalamiko ya kunyanyasa raia wakati wa uchaguzi hayatakuwepo.

Mwenyekiti wa ZEC, Khatib Mwinyichande, alisema kwa mujibu wa sheria, askari polisi ndio wanaotakiwa kulinda usalama wa raia na mali zao katika vituo vya wapiga kura.

Alisema mita 200 kutoka kituo cha wapiga kura kunatakiwa kulindwa na askari, lakini nje ya eneo hilo vikosi vingine vina haki ya kuweka ulinzi wakati wa uchaguzi.

Katika chaguzi zote zilizofanyika Zanzibar chini ya mfumo wa vyama vingi za mwaka 1995, 2000 na 2005, zilitawaliwa na vurugu huku Chama Cha Wananchi (CUF) kikililalamikia Jeshi la Polisi kwa matumizi ya nguvu na kusababisha kishindwe.

Januari 26 na 27, 2001, watu zaidi ya 30 wanaoaminika kuwa wafuasi wa CUF waliuawa na polisi wakati wakiandamana kupinga matokeo ya urais wa Zanzibar katika visiwa vya Pemba na Unguja.

***NIPASHE

.

No comments:

Post a Comment