Monday, May 31, 2010

WANAWAKE 21 WAJITOKEZA KUWANIA UONGOZI ZANZIBAR

Wanawake 21 wa Zanzibar wametangaza nia ya kugombea nafasi za uongozi kupitia vyama mbali mbali vya siasa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Oktoba mwaka huu.

Wanawake hao ni wale ambao wamenufaika na mradi wa kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi, Zanzibar (WEZA) unaoendeshwa katika Mkoa wa Kusini Unguja na Kaskazini Pemba tokea 2008.

Wanawake 13 kati ya hao wanatoka Mkoa wa Kaskazini Pemba na wanane ni kutoka Mkoa wa Kusini Unguja.

Waratibu wa Shehia za mikoa hizo wamesema wamefurahishwa na uamuzi wa wanawake hao kutaka kugombea uongozi na kwamba hayo ni maendeleo makubwa ikizingatiwa kuwa katika chaguzi zilizopita wanawake walikuwa hawajitokezi kwa wingi kugombea.

Mratibu wa Shehia ya Tumbe Magharibi, Salma Tumu, ambaye Shehia yake imetoa wanawake watano wanaogombea, amesema jitihada za kuwawezesha wanawake wa Zanzibar kujiamini kijamii na kiuchumi zikiendelezwa lengo la kupata asilimia 50 ya wanawake katika uongozi wa kuchaguliwa litafikiwa kirahisi.

Raya Majid Salim ambaye ametangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Tumbe huko Pemba amesema ameamua kugombea kwa sababu anajiamini kuwa anao uwezo wa kusimamia maendeleo ya wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo ya kijamii yanayowakabili wanawake.

“Wanawake sasa tunafahamu haki zetu katika uongozi na kilichobaki ni kuzipigania ili kuzipata na kuzitumia kwa ajili ya kuharakisha maendeleleo ya jamii nzima-wanawake, wanaume na watoto”, alisema Raya Majid Salim.

Aliyataja matatizo yanayokwamisha maendeleo ya familia na taifa huko Zanzibar ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi na viongozi kuwa ni pamoja na watoto wa kike kulazimishwa kuolewa katika umri mdogo na wanaume na wanawake wasio na kipato kukosa mitaji kwa ajili ya kuendesha miraji ya kiuchumi.

Khadija Omar Kibano ambaye anagombe udiwani wadi ya Mtambwe kaskazini amewataka wanawake nchini kote kugombea nafasi mbali mbali katika uchaguzi wa mwaka huu kama wanavyojitokeza wanaume

Mradi wa WEZA unaendeshwa kwa mashirikiano kati ya Care Tanzania, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Austria na Care Austria.
.

No comments:

Post a Comment