Monday, May 31, 2010

STARS VS BRAZIL KIINGILIO 200,000. KIWANGO CHA CHINI 30,000

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) jana lilitangaza kiingilio cha mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, na Brazil itakayopigwa Juni 7 huku kiwango cha juu kikiwa sh 200,000.

Mechi hiyo itakayopigwa siku hiyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kiwango cha chini kabisa ni shilingi 30,000.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, hadi kufikia jana, tiketi hizo za sh 200, 000 ambazo ni za jukwaa VIP A, zimekwisha.

Alisema, kulingana na idadi ya viti vya jukwaa hilo, tayari kiasi cha shilingi mil. 140 zimepatikana na kutaka wananchi wajitokeze kununua tiketi za maeneo mengine.

Mwakalebela alitaja viwango vya maeneo mengine ambapo VIP B ni sh 150,000; VIP C sh 100,000; Viti vya rangi ya chungwa mkabala na VIP, itakuwa sh 80,000 huku viti vya rangi ya chungwa, nyuma ya magoli itakuwa sh 50,000.

Alisema viwango hivyo vimetokana na gharama kubwa za kuileta timu hiyo, hivyo kuifanya mechi hiyo kuwa ya gharama kubwa tofauti na mechi nyingine zilizowahi kuchezwa nchini.

Katika hatua nyingine, mchezaji Ricardo Kaka hatacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Zimbabwe na ile itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam baada ya jana kuumizwa na
Felipe Mello katika mazoezi.

Habari zinasema, Kaka amepata maumivu makali yaliyomfanya kuibuke mzozo mkali kati yake na Mello na kumfanya Kaka kususa na kuondoka mazoezini.

1 comment:

  1. tunashukuru viongozi wetu wametuletea timu kubwa duniani lakini TFF ingejaribu kufikilia kipato cha mtanzania wa khali ya chini kwa si wote watakaoweza kulipa kiasi hicho cha pesa wafanye hata 15000 basi

    ReplyDelete