Monday, May 10, 2010

SARAFU YA EURO KUIMARISHWA

Umoja wa Ulaya pamoja na Shiriki la Fedha la Kimataifa-IMF, zimekubaliana kuanzisha mfuko wa dharura wa kiasi cha dola trilioni moja kwa ajili ya kuyaimarisha masoko ya fedha duniani na kuzuia mgogoro wa madeni wa Ugiriki usihatarishe sarafu ya Euro.

Makubaliano ya kuanzisha mfuko huo wa dharura yamefikiwa kati ya mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya, maafisa wa benki kuu na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, katika mazungumzo ya mwishoni mwa wiki mjini Brussels, Ubelgiji.

Kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno kuwahi kutengwa katika kipindi cha miaka miwili tangu kundi la mataifa 20 yaliyostawi kiviwanda-G20, lilipotoa fedha katika uchumi wa dunia kufuatia kufilisika kwa benki kubwa ya uwekezaji ya Marekani ya Lehman Brothers.
Kiasi hicho cha fedha kimewashangaza wachambuzi wa masuala ya kiuchumi na sarafu ya Euro imepanda karibu asilimia 2 huku masoko ya fedha ya Asia yakiwa thabiti.

Kufuatia tangazo hilo,Marekani na benki kuu za Japan, Ulaya, Uingereza, Canada na Uswisi zimesema zitaingilia kati kuhakikisha hakuna uhaba wa dola katika masoko ya fedha ya Ulaya. Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya fedha na uchumi, Olli Rehn, amewaambia waandishi habari kuwa Umoja wa Ulaya utailinda na kuitetea sarafu ya Euro kwa namna yoyote ile.

Hatua hizo za dharura zina thamani kubwa zaidi kuliko jitihada zozote za awali zilizowahi kuchukuliwa na nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya au na kundi la nchi 16 zinazotumia sarafu ya Euro katika kuyatuliza masoko ya fedha.
Tayari Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, zimepitisha msaada wa Euro bilioni 100 kwa ajili ya kuipiga jeki Ugiriki, ambayo nakisi ya bajeti yake ilipindukia pato lake la ndani kwa asilimia 13.6 mwaka uliopita.

Fedha hizo , dola trilioni moja zinajumuisha Euro bilioni 440 zitakazotolewa na mataifa ya Umoja wa Ulaya yanayotumia sarafu ya Euro na mkopo mwingine wa Euro 60 utatolewa na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya.
Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wamesema kuwa Euro bilioni 250 zitatolewa na IMF, hivyo kufanya jumla ya fedha hizo kuwa Euro bilioni 750 ambazo ni sawa na karibu dola trilioni moja. Kufikiwa kwa makubaliano hayo kunatokana na simu zilizopigwa jana Jumapili kati ya Rais Barack Obama wa Marekani, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.
Hata hivyo, mkurugenzi wa IMF, Dominique Strauss-Kahn hajaelezea mipango yoyote maalum, lakini amesema hatua zote za IMF zitafuata misingi ya nchi na nchi.

No comments:

Post a Comment