Monday, May 10, 2010

MAWAZIRI WA FEDHA WA EU WAKUTANA BRUSSELS

Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels wamekubaliana kuanzisha mfuko wa fedha wa hadi euro bilioni 670 kuilinda sarafu ya Euro, ili kuzuia mzozo wa madeni ulioikumba Ugiriki usisambae katika nchi nyingine zinazotumia sarafu hiyo.

Waziri wa Fedha wa Uhispania, Elena Salgado amesema kiasi hicho kinaweza kuongezeka na kufikia Euro bilioni 720, pamoja na fedha za ziada kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.

Fedha hizo zitatokana na Euro bilioni 440 zitakazotolewa na mataifa ya Umoja wa Ulaya yanayotumia sarafu ya Euro na mkopo mwingine wa Euro 60 utatolewa na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, huku Euro bilioni 220 zikitolewa na IMF.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala ya fedha na uchumi, Olli Rehn, amewaambia waandishi habari kuwa Umoja wa Ulaya utailinda na kuitetea sarafu ya Euro kwa namna yoyote ile.

Taarifa za mkopo huo wa fedha wa Umoja wa Ulaya umeisababisha Euro kuongezeka hadi dola 1.29 katika masoko ya fedha ya Asia hii leo.

.

No comments:

Post a Comment