Thursday, May 20, 2010

MWAKILISHI WA HRW AFUKUZWA BURUNDI

Serikali ya Burundi imefuta kibali cha kufanya kazi nchini humo,kwa mwakilishi wa Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu-Human Rights Watch, Neela Ghoshal. Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Burundi imemwandikia barua Bibi Ghoshal ikimtaka asimamishe shughuli zake mara moja na kuondoka nchini humo ifikapo tarehe 5 mwezi ujao wa Juni.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya shirika hilo wiki iliopita kuchapisha taarifa kuhusu vurugu zinazoendelea Burundi kabla ya uchaguzi mkuu. Serikali ya Burundi imesema miongoni mwa mambo mengine, ripoti hiyo iliegemea upande mmoja ikiwa dhidi ya serikali na chama tawala. Shirika hilo limeelezea kusikitishwa kwake na uamuzi huo uliochukuliwa dhidi ya Ghoshal.

Mwezi Desemba, mwaka jana Burundi ilimfukuza nchini humo mkuu wa zamani wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi-BINUB, Youssef Mahmoud, kwa madai alikua karibu sana na upande wa upinzani. Maafisa wengine wawili wa Umoja wa Mataifa walifukuzwa nchini humo mwaka 2006 kwa madai sawa na hayo.

No comments:

Post a Comment