Friday, May 21, 2010

10 WAOKOLEWA AJALI YA BOTI ZANZIBAR

Watu 10 wameokolewa baada ya mashua ya MV Muafaka kuzama ikiwa na magunia 200 ya mkaa katika mwambao wa Makoongwe Kisiwani Pemba.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hassan Nassir, alisema watu hao pamoja na wafanyakazi wa boti hiyo, waliokolewa juzi na boti ya wavuvi iliyokuwa ikielekea Mombasa nchini Kenya.

Alisema boti hiyo ya wavuvi iliwaona watu hao wakielea baharini na ndipo walipoamua kutoa msaada huo wa kuwaokoa na kuwapeleka katika kisiwa cha Kokota, Mkoa wa Kaskazini Pemba kabla ya kuchukuliwa na boti ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM).

Hata hivyo, alisema mtu mmoja, Khalid Hassan, alipoteza nguvu na kuzama baharini wakati juhudi za kuwaokoa zilipokuwa zikifanyika katika eneo hilo.

Aliwataja abiria waliookolewa kuwa ni Ramadhani Abdallah (30), mkazi wa Mapinduzi, Said Juma Bakari (26), mkazi wa Mtambwe, Juma Haji Silima (54), mkazi wa Mtuhaliwa, Mcha Haji (22), mkazi wa Mkoani na Mohammed Khamis Muhidini (65), mkazi wa Mtuhaliwa na Hassan Ali Hassan (21).

Pia aliwataja mabaharia waliokolewa katika chombo hicho kuwa ni Khamis Suleiman Mohammed, Shaibu Khamis Faki, Ali Bakari na Khamis Hassan Mwalimu akiwemo pamoja na nahodha wa chombo hicho.

Kamanda Nassiri alisema nahodha wa chombo hicho aliachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea kufanyika kuhusiana na tukio hilo.

Aidha, alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mashua hiyo ilikuwa na abiria 11.

Alifafanua kuwa mashua hiyo ilisajiliwa kwa kazi ya kubeba mizigo lakini nahodha huyo alibeba abiria saba katika chombo hicho.

Alisema mashua hiyo ilipakia magunia 200 ya mkaa katika kijiji cha Fumbani lakini baada ya kufika katika mwambao wa Makongwe, chombo hicho kilianza kuingiza maji na kulazimika kurudi walikotoka kabla ya kuzama.

Hata hivyo, Kamanda Nassiri aliwataka wananchi kujiepusha kutumia usafiri wa vyombo vya baharini visivyokuwa na usalama wa maisha yao.

Kisiwa cha Pemba kimekabiliwa upungufu wa usafiri tangu meli za Serikali MV Mapinduzi na MV Maendeleo kusimama kutoa huduma kutokana na uchakavu na meli ya MV Serengeti kuwaka moto ikiwa imetia nanga katika Bandari ya Malindi, Zanzibar.

No comments:

Post a Comment