Tuesday, May 4, 2010

KARUME ASAINI SHERIA YA KURA YA MAONI ZANZIBAR


Rais Amani Abeid Karume, amesaini sheria ya kuweka masharti ya kura ya maoni itakayoamua kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Akizungumza na Nipashe, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alisema Rais Karume aliusaini muswada huo Aprili 30 baada ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitisha sheria hiyo.

“Tayari Rais Karume amesaini sheria ya kuruhusu kuitishwa kura ya maoni, imebakia hatua ya pili ya kutangaza siku ya kufanyika kura ya maoni,” alisema Kificho.

Alisema Baraza la Wawakilishi tayari limeshapokea hatua hiyo ya utekelezaji wa Rais wa kusaini sheria hiyo.

Alieleza kuwa baada ya hatua hiyo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ndio itakayosimamia kura ya maoni, baada ya Rais kutangaza siku ya kufanyika kwa kura hiyo.

Kificho alisema kamati ya watu sita ya Baraza la Wawakilishi yakufuatilia utekelezaji bado haijaanza kazi yake kutokana na baadhi ya mambo kuwa bado hayajakamilika.

“Nipo katika kukamilisha majukumu yatakayofanywa na kamati, baada ya kukamilika kamati hiyo itaanza kazi mara moja,” alisema Spika Kificho.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, alisema ni mapema kuzungumza lini kura ya maoni itafanyika hadi hapo Rais atakapotangaza.

Alisema wananchi walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ndio watakaoshiriki kupiga kura ya maoni.

Mkurugenzi huyo alisema zoezi la uandikishaji wapiga kura katika daftari hilo limekwenda vizuri na kesho ndio siku ya mwisho wa uandikishaji.

Suala la kuitishwa kwa kura ya maoni kabla ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa liliamriwa kwenye kikao cha Halimashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM iliyokutana Butiama mwishoni mwa Machi, 2008 kwa maelezo kuwa suala hilo linahusu katiba ya nchi.

Uamuzi wa kufikia maelewano na kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar ulifikiwa na Rais Karume na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, Novemba 5, mwaka jana.

Viongozi hao walifikia makubaliano hayo baada ya kukutana Ikulu na baadaye Maalim Seif alifanya mikutano kadhaa Unguja na Pemba kuwaelezea wafuasi wa CUF kuhusiana na uamuzi huo wa kumaliza uhasama na kumtambua Rais Karume.

Baada ya hapo Mwakilishi wa Mgogoni, Abubakar Khamis Bakari, aliwasilisha hoja binafsi katika Baraza la Wawakilishi Februari mwaka huu, akitaka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao.

Baraza hilo lilipitisha uamuzi huo katika mkutano uliopita kabla ya kusainiwa na Rais Karume.

.

No comments:

Post a Comment