Tuesday, May 4, 2010

MSHUKIWA WA JARIBIO LA KURIPUA MABOMU AKAMATWA NEW YORK

Maafisa wa uchunguzi nchini Marekani walimtambua Faisal Shahzad kama mzaliwa wa Pakistan na ambaye ni raia wa Marekani. Mwanasheria mkuu, Eric Holder, akitangaza kukamatwa huko kwa Faisal alisema uchunguzi unaimarishwa kutathmini ikiwa alikuwa akishirikiana na makundi ya kigaidi.

Duru za habari zinasema kwamba Faisal mwenye umri wa miaka thelathini, aliishi katika mkoa wa Connecticut, nchini Marekani, na hivi karibuni alirejea kutoka mji wa Peshawar nchini Pakistan kwa ziara ya miezi mitano. Peshawar ni mji unaoshukiwa kuwa ngome ya kutoa mafunzo kwa makurutu wa makundi ya Al-Qaeda na Taliban.

Taarifa kutoka katika idara ya polisi ilisema mshukiwa huyo alitiwa kizuizini saa sita kasorobo usiku wa Jana kwa madai ya kuendesha gari lililotegewa bomu katika eneo la Times Square na haikufafanua mashtaka kamili yanayomkabili.

Maafisa wa polisi walichukua hatua za dharura na kuwaondosha maelfu ya watu wakiwemo watalii waliotaka kurejea katika hoteli zao muda mfupi baada ya njama hiyo ya kuripua bomu ilipotibuka. Mwanasheria mkuu nchini Marekani, Eric Holder, alisema Faisal Shahzad alikamatwa katika uwanja wa ndege wa J.F. Kennedy alipokuwa akijaribu kupanda ndege iliyokuwa ikielekea mjini Dubai. Alisema maafisa wa shirika la upelelezi la FBI na pia waendesha mashtaka walihusika katika uchunguzi.

Bw, Holder alisema jaribio hilo la kigaidi lilikuwa na madhumuni ya wazi ya kuwauwa Wamarekani. Faisal anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kufunguliwa mashtaka ambayo hayakufafanuliwa.

Kamishna wa polisi mjini New York, Ray Kelly, alisema huenda jaribio hilo lilihusisha washukiwa wengi. Kulingana na maafisa wa uchunguzi, mshukiwa huyo alinunua gari lililokuwa na bomu wiki moja kabla ya tukio hilo la Jumamosi.

Mji wa New York umekuwa ukiangazwa zaidi kutokana na kitisho cha miripuko tangu shambulio la Septemba 11 mwaka wa 2001 katika jumba la World trade centre lililowauwa kiasi ya watu 3000.

Kufikia sasa kundi la wapiganaji wa Pakistan la Tehreek-e-Taliban ndilo limejitokeza kudai kuhusika na jaribio hilo la kutaka kuripua bomu.



.

No comments:

Post a Comment