Thursday, April 8, 2010

UJERUMANI YAIPA TANZANIA MSAADA WA EURO MILIONI 8.5

Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel na Waziri wa Fedha na Uchumi wa Tanzania, Mustafa Mkulo, leo wametia saini msaada wa Euro milioni nane na laki tano uliotolewa na Ujerumani kwa ajili ya kusaidia taasisi zisizo za kiserikali, sekta ya afya na huduma ya maji. Msaada huo umesainiwa jijini Dar es Salaam, ambako Bwana Niebel amesema Tanzania imekua ikijitahidi kuinua uchumi wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema mkutano wake na viongozi wa Tanzania ulijadili tatizo la maharamia wa Somalia katika bahari ya Hindi.

Asubuhi ya leo, mawaziri hao waliitembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam, na kuzindua mashine muhimu ya uchunguzi kwa ajili ya wagonjwa wa saratani iliyotolewa kama msaada na Ujerumani.

Pia leo jioni, Waziri Westerwelle alifungua rasmi Taasisi ya utamaduni wa Kijerumani ya Goethe jijini Dar es salaam.

Taasisi ya Utamaduni wa Kijerumani ya Goethe pamoja na mambo mengine, hutoa pia mafunzo ya lugha ya Kijerumani.

Ujerumani na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa karibu kwa muda mrefu, hivyo kuzinduliwa kwa kituo hicho kunaimarisha mahusiano ya karibu baina ya wananchi wa nchi hizo mbili.


.

No comments:

Post a Comment