Thursday, April 8, 2010

WESTERWELLE NA NIEBEL WAIZURU TANZANIA

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, leo amekutana na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, kituo chake cha kwanza cha ziara yake ya siku tano barani Afrika.

Katika ziara hiyo, Westerwelle ameongozana na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, ambaye pia atafanya mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri wa Fedha na Uchumi wa Tanzania, Mustafa Mkulo.

Waziri Westerwelle amesema bara la Afrika linakabiliwa na matatizo mengi, lakini pia lina nafasi nyingi za kuweza kufaulu. Kiongozi huyo aidha amesema Ujerumani inataka kushiriki kikamilifu katika kuzitumia nafasi hizo, kwa maslahi ya bara la Afrika, Ujerumani na Ulaya.

Ndio maana Ujerumani ina sera ya kigeni inayozingatia zaidi nafasi za kiuchumi na ina majukumu makubwa ya kibinadamu barani Afrika.

Waziri Westerwelle anatambua kwamba bara la Afrika lina tofauti kubwa ndio maana amesisitiza haja ya kuwa na mikakati maalum kwa kila sehemu ya bara hilo.

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel kwa upande wake amesema ni muhimu kwamba amefanya ziara hiyo pamoja na waziri wa mambo ya kigeni Guido Westerwelle, kwa kuwa katika miaka iliyopita Ujerumani ilichukua hatua mbalimbali katika mataifa yaliyo washirika wake.

Amesema anaamini ni jambo la manufaa makbuwa kwa Ujerumani na washirika wake kwa wizara za misaada ya maendeleo na wizara ya mambo ya kigeni kufanya kazi chini ya mwavuli mmoja.

Waziri Niebel amesema, "Tunakata ifahamike nchini Ujerumani kwamba Afrika ni bara lenye nafasi nzuri za ufanisi mkubwa na kama mtu hatawekeza katika bara hili basi atakuwa anakosa nafasi hii muhimu."

Asubuhi ya leo waziri Westerwelle na waziri Niebel waliitembelea taasisi ya saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, na kuzindua mashine muhimu ya uchunguzi kwa ajili ya wagonjwa wa saratani iliyotolewa kama msaada na Ujerumani. Akizungumza na idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle, mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, bwana Twalib Ngoma, amesema mashine hiyo itawasaidia kupanga matibabu.

Waziri Westerwelle anatarajiwa kukutana na rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Rwanda-ICTR, jaji Dennis Byron. Baadaye pia anatarajiwa kuifungua rasmi taasisi ya utamaduni wa Kijerumani ya Goethe mjini Dar es salaam leo jioni.

Mawaziri hao wawili watazitembelea pia Afrika kusini na Djibouti.

.

No comments:

Post a Comment