Saturday, April 3, 2010

SMZ, WAMILIKI WA DALADALA WAVUTANA

Mvutano umejitokeza kati Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na wamiliki wa daladala, baada ya wamiliki hao kupandisha nauli huku serikali ikipinga viwango vipya.

Mvutano huo umeibuka baada daladala katika Manispaa ya Zanzibar kupandisha nauli kutoka Sh. 250 hadi 400 kwa madai ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Baadhi ya makondakta wa daladala wa kituo cha mabasi darajani, walisema kuwa mafuta yamepanda kwa muda wa wiki moja sasa na haiwezekani kuendelea kutumia viwango vya zamani vya nauli.

Walisema daladala zinazokwenda njia ya Fuoni, abiria wanalazimika kulipa Sh. 350 badala ya 250, Chukwani na Uwanja wa Ndege Sh. 300 badala ya Sh. 250 wakati Bububu ni Sh. 400 kutoka Sh. 250.

“Suala la kupandisha bei halina mjadala, tunachoomba wananchi wakubaliane na viwango vipya vya bei kwa sababu serikali imekubali kupandishwa bei ya mafuta, alisema, Mrisho Kombo, kondakta wa daladala.

Nauli nyengine zilizopanda ni magari yaendayo vijijini kama Mkokotoni, Nungwi, Kiwengwa, Matemwe na Bumbwini, ambapo zimeongezeka kwa Sh. 200.

Abiria wendao kijiji cha Nungwi awali walikuwa wakitozwa 1500 lakini tangu kuanza bei hiyo wanalipishwa Sh. 1700, Kiwengwa Sh.1500 kutoka Sh. 1300 na Mkokotoni Sh. 1250 kutoka Sh.1000.

Hata hivyo, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othman Said, alisema ni marufuku kutumika viwango hivyo vipya kwa kuwa havina baraka za serikali.

Alisema serikali bado haijatangaza viwango vya nauli licha ya mafuta kupanda na kufafanua kuwa inapotokea hali kama hiyo, serikali hukaa na wadau wa usafirishaji kabla ya viwango vipya kupandishwa.

Alisema baada ya kumalizika kwa mapumziko ya Pasaka, Idara ya Usafirishaji na Leseni Zanzibar itakutana na wadau na kwamba mwananchi ambaye atatozwa nauli mpya ana haki ya kuchukua namba ya gari husika na kuripoti katika Idara ya Leseni na Usafirishaji ili hatua za kisheria zichukuliwe.

***Nipashe

.

No comments:

Post a Comment