Saturday, April 3, 2010

ALIYEKUTWA NYUMBANI KWA MWAKANJUKI HAJUILIKANI ALIKO

Na Romana Mallya

Hatma ya Aboubakar Mohamed (22) ambaye alikutwa hivi karibuni uchi wa mnyama nje ya geti la Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Brigedia Jenerali Adam Mwakanjuki, imeendelea kuwa tete kutokana na kutojulikana alipo hadi sasa.

Mohamed ambaye inadaiwa kuwa ni mwenyeji wa mkoa wa Tanga, Machi 12, mwaka huu alikutwa na wananchi nje ya geti la waziri huyo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na kudai kuwa alikuwa anawasubiri wenzake waliokuwa ndani ya nyumba ya waziri.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Sebastian Masinde, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema kuwa baada ya kumkamata mtu huyo siku ya tukio walimfikisha kituoni kwa mahojiano.

Alisema wakati wa mahojiano mtu huyo alionekana kutojitambua.

“Wakati wa mahojiano alipotakiwa kutaja majina yake, alilitaja la Mohamed na alipotakiwa kulitaja jila la pili, aliwaambia polisi kuwa wampe soda ndipo afanye hivyo.

Kutokana na hali yake, tuliamua kumpeleka hospitali ya Mwananyamala,” alisema.

Aidha, alisema walipata taarifa kuwa Mwanyamala walimuhamishia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

“Ninachojua ni kwamba tulimpeleka Hospitali ya Mwananyamala na baadaye alihamishiwa Muhimbili, jaribu kuulizia huko,” alisema.

Afisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema wao hawajampokea mtu mwenye jina hilo.

Alisema kwa siku hupokea wagonjwa wengi na kwamba mwenye jina hilo hayupo.

“Labla kama Mwananyamala walivyomleta kwetu hawakumwandika jina, unajua wagonjwa wengi wa akili wanapoletwa hospitalini hapa mara nyingi wanakuwa hawana majina,” alisema.

Mwandishi alipokwenda Mwananyamala, alijibiwa kuwa kwa siku hospitali hiyo hupokea wagonjwa wengi hivyo hawana kumbukumbu.

Mmoja wa majirani wa eneo hilo, Eminiana Mwanambuu, alisema kuwa alimuona mtu huyo wakati akielekea dukani.

Mwanambuu alisema kutokana na tukio hilo, aliamua kumwita jirani mwenzake ili waweze kumuhoji mtu huyo.

Alisema katika mahojiano mtu huyo alidai kuwa, alitokea Shelisheli na alikuwa akielekea Namibia na wenzake watatu kwa kutumia usafiri wa ndege ambayo waliiacha juu ya mti.

Aidha, mtu huyo aliwaeleza watu kuwa wenzake aliokuwa nao wapo ndani ya nyumba ya Brigedia Jenerali Mwakanjuki na kwamba wapo huko kwa lengo la kuomba kikombe cha maji ambayo ni lazima yatolewe na mke wa Mwakanjuki.


.

No comments:

Post a Comment