Wednesday, April 28, 2010

OCEAN VIEW YAPAA LIGI YA ZANZIBAR


BAO pekee la Nassor Ali, limeiwezesha timu yake ya Zanzibar Ocean View kuibuka na ushindi katika mchezo wa ligi kuu ya Zanzibar dhidi ya vibonde wa ligi hiyo, Konde Star.

Zanzibar Ocean View sasa imechupa kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili katika msimamo wa ligi na kuwashusha mabingwa watetezi Mafunzo.

Mafunzo yenye pointi 15 ilikuwa ikikamata nafasi ya pili mbele ya vinara KMKM wenye pointi 18, lakini kwa ushindi wa juzi dhidi ya Konde umeifanya Zanzibar Ocean View kufikisha pointi 17.

Katika mchezo huo uliopooza na kuhudhuriwa na mashabiki wachache ilishuhudiwa timu ya Konde ikiendelea kugeuzwa kapu la magoli.

Zanzibar Ocean View hivi karibuni ilijipatia pointi za mezani baada ya Chama cha soka Zanzibar ( ZFA) kuipa pointi tatu kufuatia rufani yake iliyoikatia Miembeni kupita, hivyo inazidi kujisogeza katika kinyang'anyiro cha timu zinazogombea ubingwa wa soka Zanzibar msimu huu.

Konde ambao nao wamepanda daraja msimu huu, hadi sasa ikiingia mzunguko wa pili wa ligi hiyo ipo katika hatihati ya kubaki katika ligi mwakani kutokana na kufanya vibaya kwenye mechi zake.

Timu hiyo hadi sasa ina pointi tano katika mechi 12 ilizocheza.

.

1 comment:

  1. Ningependa utoe msimamo wa ligi upo vipi zanzibar.

    ReplyDelete