MWANACHAMA wa chama chochote cha siasa kilicho na usajili visiwani hapa, anayetaka kuwania urais, atatakiwa kuwa na Sh milioni tatu ili aweze kupata fomu za kuwania nafasi hiyo ya juu nchini.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imetangaza rasmi gharama hiyo na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Khatib Mwinyichande, kiasi hicho kimepanda kutoka Sh milioni moja za mwaka 2005.
Alisema wagombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, watachukua fomu kwa Sh 300,000, wakati wa usheha, watalipa Sh 50,000. Katika uchaguzi wa mwaka 2005, wawakilishi walilipa Sh 50,000 kwa fomu huku usheha ukilipiwa Sh 15,000 kwa fomu.
Mchakato wa kuwania urais katika uchaguzi huo Visiwani hapa, unatarajiwa kufanyika kwa siku 20 kuanzia Agosti 10 mwaka huu.
Mwinyichande alisema siku tano baadaye, itaanza ngwe nyingine, kwa ajili ya wanaowania kuingia katika Baraza la Wawakilishi. Mchakato wao unatarajiwa kuwa wa siku 15.
“Kampeni za Uchaguzi Mkuu zitaanza Septemba 10 na kufikia kikomo jioni ya Oktoba 30,” alisema Mwinyichande aliyethibitisha kwamba, uchaguzi utafanyika Oktoba 31, siku ambayo nchi nzima ya Tanzania itakuwa katika uchaguzi.
Aidha, ZEC inatarajiwa kutangaza rasmi matokeo ya uchaguzi huo Novemba 2, mwaka huu. Mwinyichande alisisitiza kwamba, ZEC iko katika harakati za kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki.
Wakati huohuo, kundi la Wazanzibari 12 wanaojiita 'Wawakilishi wa Watu wa Zanzibar’, liliibuka jana na kushikilia msimano wa kupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wakidai kuwa “si halali na lazima utenguliwe.”
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, viongozi wa kundi hilo, Yussuf Mchenga, Amour Mbamba na Rashid Ahmed, walisema wanaendelea na harakati za kisheria kuhakikisha wanauvunja Muungano huo ambao keshokutwa unatimiza miaka 46.
“Barua yetu tuliyoituma Umoja wa Mataifa (UN) imepokewa rasmi, sasa tunasubiri majibu kabla ya kwenda mahakamani. “Tunataka Mamlaka husika ya UN ithibitishe uhalali wa Muungano huu au iuvunje,” alisema.
Ahmed alisema katika harakati za kufungua kesi, wanasheria wakuu wa Tanzania na Zanzibar, Katibu Mkuu wa UN kati ya mwaka 2005 na 2006, walishindwa kuonesha mkataba wa kuundwa kwa Muungano.
Hata hivyo, wasemaji hao wa kundi hilo walikataa kueleza kilichomo katika barua yao UN na hata kueleza chanzo cha fedha inayowapa jeuri ya kutaka kufungua kesi dhidi ya Muungano.
Katika hatua nyingine, wasemaji hao walimpongeza Rais Amani Karume kwa juhudi zake za kutaka kuhakikisha suala la mafuta na gesi ya asili visiwani hapa linaondolewa katika masuala ya Muungano.
.
No comments:
Post a Comment