Friday, April 23, 2010

SERIKALI KUONDOA GHARAMA ZA KUUNGANISHA UMEME

WIZARA ya Nishati na Madini imesema inaangalia uwezekano wa kuondoa gharama anazotozwa mwananchi wa kawaida pindi anapokwenda kuomba huduma ya kuunganishiwa umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ilemela, Athony Diallo (CCM), aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani za kuwapungizia wananchi mzigo huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, alikiri kuwepo tatizo hilo na kusema serikali inaliangalia.

“Mheshimiwa Spika ni kweli kumekuwepo na malalamiko haya kwa kipindi kirefu mno, sasa umefika wakati ambao tutashauriana na mamlaka husika, ili kuondoa tatizo hili,” alisema Waziri Malima.

Alisema katika utaratibu huo, wateja wa shirika hilo wamekuwa wakitakiwa kununua waya na vitu vingine hata kabla ya kufungiwa umeme.

“Utaratibu huu umechukua muda mrefu mno, si utaratibu mzuri; unapaswa kuangaliwa upya… kwa manufaa ya Watanzania wote,” alisema Waziri Malima.

Alikuwa akijibu swali la msingi lilioulizwa na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Dk. Charles Mlingwa (CCM) kwamba TANESCO itapeleka lini umeme katika vijiji vya Kizumbi, vitongoji vya Nhelegani na Bugayambelele.

Alisema katika maeneo hayo kuna transfoma mbili ambazo zinahudumia wateja watano tu na mashine moja ya kusaga ya Chuo Kikuu cha Ushirika.

Alisema kutokana na hali halisi iliyopo sasa ya uwezo wa serikali, haitakuwa rahisi kugharamia mahitaji yote ikiwa ni pamoja na kupeleka umeme kwenye shule za sekondari.

Alisema utaratibu uliopo ni kuainisha upelekaji au kufikisha huduma hii kwa shule pale ambapo kazi inakuwa sehemu ya mradi wa kusambaza umeme.

.

No comments:

Post a Comment