Monday, April 5, 2010

IKULU ZNZ YAICHAPA IKULU BARA 3-1 NI KATIKA KUSHEREHEKEA PASAKA

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, Michael Mwanda amesema kuwa mashindano ya mwaka huu ya michezo ya Pasaka kati ya Ikulu hiyo na Ikulu ya Rais, Zanzibar yamechangia kuimarisha, kuuenzi na kuudumisha Muungano wa Tanzania.

Aidha, Katibu Mkuu huyo ametaka mashindano hayo, ya kwanza kati ya timu za Ikulu hizo katika historia ya Tanzania, yaendelezwe na kuimarishwa kwa kushirikisha michezo zaidi na kuundwa kwa timu za viongozi na wakuu wa idara za Ikulu hizo mbili.

Mwanda alikuwa akizungumza kwenye hafla ya chakula cha usiku ambacho Klabu ya Michezo ya Ikulu, Dar es Salaam, iliwaandalia wageni wao kutoka Zanzibar kwenye Ukumbi wa Mhasibu House, Dar es Salaam, juzi Jumamosi.

Hafla hiyo ya chakula cha usiku ilihudhuriwa na wanamichezo kutoka Ikulu zote mbili za Dar es Salaam na Zanzibar, viongozi wao, na viongozi wa Ikulu Sports Club wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Frank Mganga, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Ikulu, Dar es Salaam.

Mwanda aliwaambia wanamichezo na viongozi wao: "Michezo ya leo, imesaidia kulinda zaidi afya zetu, imetukutanisha na kuweza kufahamiana, imejenga urafiki na undugu baina yetu, imeanzisha mawasiliano endelevu, na zaidi ya yote kwetu sisi hapa leo imekuwa ni moja ya njia za kuimarisha, kuuenzi na kuudumisha Muungano wetu.”

Timu ya Ikulu, Zanzibar iliwasili Dar es Salaam Alhamisi iliyopita kwa mwaliko wa Ikulu Sports Club, na jana timu hizo zilichuana katika michezo ya soka, netiboli, kuvuta kamba na kufukuza kuku kusherehekea Sikukuu ya Pasaka.

Ikulu Zanzibar ilishinda mchezo wa soka kwa mabao 3-1 na pia ikashinda mchezo wa kufukuza kuku. Ikulu Dar es Salaam ilishinda katika mchezo wa netiboli 22-17 na pia ikashinda mchezo wa kuvuta kamba. Mwanda amewashauri viongozi wa timu hizo mbili kuhakikisha kuwa michezo ya mwakani, ambayo itafanyika Zanzibar, inashirikisha pia viongozi na Wakuu wa Idara wa Ikulu hizo mbili.

"La muhimu zaidi na ambalo litaleta msisimko wa kutosha ni kwa viongozi, yaani Wakuu wa Idara wa pande zote mbili za Muungano kuunda timu zitazofungua dimba la mashindano ya miaka ijayo.”

Bwana Mwanda pia ametaka mashindano hayo yaimarishwe kwa kuongeza michezo mingine na hivyo kuleta msisimko mkubwa zaidi. "Aidha, mahusiano haya yaimarishwe na kuboreshwa ili siku za usoni tuwe na michezo mingi zaidi na yenye msisimko zaidi.”

Wanamichezo hao wa Zanzibar ambao walitwaa ushindi huo mnono na kukabidhiwa zawadi ya misalaba wanatarajiwa kuondoka Dar es Salaam leo kurejea kwao.


.

No comments:

Post a Comment