Friday, March 26, 2010

YAHYA HUSSEIN AJA NA "UZUSHI" MPA

Mtabiri maarufu katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein ameibuka na utabiri mpya kuwa mwaka huu uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani hautafanyika kama ilivyopangwa.

Sheikh Yahya alitoa utabiri huo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Hata hivyo, alipotakiwa na waandishi kutoa maelezo zaidi kuhusu utabiri huo alisema kwamba anapotoa utabiri hatakiwi kutolea majibu.

Aidha alisema baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo tofauti na utabiri wake huku wengi wakidhani anatumiwa na viongozi wa kisiasa.

“Kwanza napenda kuwafahamisha kwamba mimi ninapotoa utabiri wangu huwa simlengi mtu wala simtabirii mtu, natoa utabiri kwa manufaa ya jamii. Kwa hiyo ni wajibu wa kila mtu aidha kukubali au kukataa haya ambayo ninayasema,” alisema Sheikh Yahya.

Alisema kwa upande wa Zanzibar, Rais Amani Abeid Karume ataendelea kuongezewa muda wa kutawala tofauti na wengi wanavyofikiria.

Kuhusu Bunge, mtabiri huyo alisema bunge lijalo litakuwa na sura nyingi mpya huku wanawake wakiongezeka kwa idadi kubwa wakati robo tatu ya wabunge wa zamani watapoteza nafasi zao.

Sheikh Yahya, alisema kinyota watu watakaokuwa na bahati ni wale wanaoanzia na herufi za majina ya ‘S’.

Kutokana na hali hiyo, alisema nyota ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta itaendelea kung’ara na kwamba hakuna mtu atakayemchezea katika masuala ya siasa.

Alisema kitendo cha kupatwa kwa jua Januari 15, 2010, kunaashiria kuwepo kwa vurugu, umwagikaji wa damu, harakati za kijeshi na kashfa za kipolisi, mabadiliko ya uongozi katika ngazi mbalimbali, uasi wa ghafla katika serikali za nchi ambazo zilipitiwa na kupatwa kwa jua.

“Nchi za Chad, Somalia, Tanzania, Kisiwa cha Zanzibar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, India, Sri Lanka, Bangladesh na Mayanmar ndizo zilizopitiwa na kupatwa kwa jua vile vile kutokea vurugu za uchaguzi katika nchi hizo, watu kufanya maasi na matukio ya kigaidi,” alisema Sheikh Yahya.

Akizungumzia kuibuka kwa Chama Cha Jamii (CCJ), alisema kitakuwa kimedhamiria kukimaliza Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini jamii inatakiwa kufahamu kuwa CCM itaweza kuvunjwa na wanachama wenyewe na si chama chochote cha siasa.

“CCJ ilitakiwa kutafuta ushauri wa kinyota. Iwapo CCJ ingejiita CCN hapo kungekuwa na uwezekano wa kuishinda CCM, lakini kutokana na kukosea kuchagua herufi basi chama hicho hakikiwezi kabisa chama tawala hata wakitumia jina la Baba wa Taifa Julius Nyerere,” alisema.

Sheikh Yahya ameibuka na utabiri huo baada ya hivi karibuni kutabiri kuwa kama kuna mwanachama au mwanasiasa atayakayejitokeza ndani ya CCM kumpinga Rais Jakaya Kikwete katika mbio za urais mwaka huu, atakufa ghafla.


.

No comments:

Post a Comment