Friday, March 26, 2010

JK NA RONALDO, MKAPA NA WAANDISHI WA NJE


Na Johnson Mbwambo.

Nilijizuia mno nisiandike chochote kuhusu tukio la Jumanne ya wiki iliyopita ambapo Rais wetu, Jakaya Kikwete, ‘alizawadiwa’ jezi ya Ronaldo na Rais wa Klabu ya Real Madrid ya Hispania, Florentino Perez.

Ilielezwa wakati wa hafla hiyo ya Ikulu kwamba bwana mkubwa huyo wa Real Madrid ameamua ‘kumzawadia’ Kikwete jezi hiyo ikiwa ni ‘kuthamini’ mchango wake katika kuinua kandanda (sijui ni kuinua Taifa Stars au Real Madrid!).

Picha za Kikwete akipokea jezi hiyo Na. 9 ya Ronaldo zilipamba kurasa nyingi za michezo za magazeti yetu nchini, Jumatano ya Machi 17. Naomba Mungu ili Kikwete asije, siku moja, kuivaa jezi hiyo; maana tumewahi kumwona Pinda akiwa amevaa fulana ya Vodacom!

Nasema nilijizuia sana nisiandike chochote kuhusu tukio hilo; japo nilipokea e-mail nyingi za wasomaji wangu wa Ughaibuni (wasomaji wa hapa nchini labda waliona ni tukio la kawaida) zilizoonyesha kukerwa kwao na tukio na picha hiyo.

Sababu za kujizuia nisiandike chochote kuhusu tukio hilo ni nyingi, lakini kubwa ni malalamiko kutoka kwa baadhi ya wana CCM kwamba namwandama mno Rais Kikwete katika safu yangu kwa mambo madogo madogo! Wanasahau kuwa katika maisha ni mambo madogo madogo ambayo mwisho wa yote hujenga picha kubwa ya hulka ya mtu.

Hata hivyo, uvumilivu huo uliniishia jioni ya Alhamisi iliyopita, Machi 18, nilipomsikia Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa akihojiwa mjini Nairobi na BBC na kulalamika kwamba tatizo kubwa linaloikabili Tanzania ni ukosefu wa uzalendo!

Mkapa, ambaye alikuwa Kenya kuhudhuria maadhimisho ya miaka 50 ya Kampuni ya Nation Media Group, alitumia fursa hiyo kuwaponda sana waandishi wa habari wa Tanzania, na kujisifu kwamba yeye wakati wa urais wake alikuwa akipenda zaidi kuzungumza na waandishi wa habari wa nje!

Akizungumza kwenye ukumbi uliofurika wageni mbalimbali, wakiwemo Rais Kibaki na Rais Kagame, Bw. Mkapa aliwaponda waandishi wa Tanzania kwamba hawana uelewa wa kutosha wa masuala mbalimbali.

Hata hivyo, hiyo si mara ya kwanza kwa Mkapa kuwaponda waandishi wa habari wa Tanzania; japo safari hii amewaponda akiwa mbele ya marais wengine wawili (Kagame na Kibaki) ambao wao walisema katika mkutano huo kuwa wana kawaida ya kuzungumza na waandishi wa nchi zao!

Baadaye jioni, Bw. Mkapa alihojiwa na BBC kuhusu mahusiano ya waandishi wa habari na marais; hususan wa Afrika Mashariki, na ndipo aliposema kwamba mahusiano hayo ni muhimu lakini akasisitiza kuwa tatizo kubwa linaloyakwaza, ni ‘ukosefu wa uzalendo’. Karibu mara mbili tatu hivi wakati wa mahojiano hayo, Bw. Mkapa alirudia suala hilo la ‘ukosefu wa uzalendo’.

Ni kwa muktadha huo nashawishika leo kuyalinganisha matukio hayo mawili ya Nairobi na Dar es Salaam ya Bw. Mkapa na Rais Kikwete, kwa sababu, kwa mtazamo wangu, yafananafanana.

Wakati Mkapa anajisifu, mjini Nairobi, kwamba anapenda kuzungumza na waandishi wa habari wa nje na si wa Tanzania; huku hapo hapo akibainisha kwamba tatizo kuu linaloikabili nchi yetu ni ‘ukosefu wa uzalendo’; mjini Dar es Salaam nako Rais wetu Kikwete alikuwa akihudhuria, Ikulu, hafla ya kukabidhiwa ‘zawadi’ ya jezi ya mchezaji wa klabu ya Hispania – Ronaldo!

Kama ‘uzalendo’ ndiyo kigezo chetu kikuu cha kutathmini matukio hayo mawili ya Nairobi na Dar es Salaam; nashawishika kuuliza: Ni nani kati ya Kikwete na Mkapa tunayeweza kusema alionyesha uzalendo katika matukio hayo mawili tofauti?

Je, ni Kikwete anayekubali kukaribisha, Ikulu, hafla ya kukabidhiwa jezi ya mwanasoka wa Hispania (Ronaldo) au ni Mkapa anayejisifu ugenini kwamba yeye hupendelea kuzungumza na waandishi wa habari wa Ughaibuni tu (Ulaya na Marekani)?

Ndugu zangu; ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba, ni kweli tuna tatizo la ukosefu wa uzalendo; lakini wachangiaji wakubwa wa ukosefu huo wa uzalendo nchini mwetu, ni watawala wetu wenyewe.

Unapokuwa na rais wa nchi ambaye anakubali, katika hafla rasmi ya Ikulu, ‘kuzawadiwa’ jezi ya Ronaldo maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba anatuma ujumbe kwa vijana wetu wadogo mashuleni na hata kwa sisi wazee wazima, kwamba, hata kwenye michezo, nyota wa nje ndiyo wa kuwathamini na wa kuwapapatikia.

Kwa mtazamo wangu, ujumbe ulio dhahiri alioutuma ni ule wa kuthamini vya nje (vya wazungu), na si vya kwetu. Sasa kama hali ni hiyo, ni vipi tunaweza kujenga uzalendo kama hata viongozi wetu wenyewe wanawapapatikia na kuwatukuza wanamichezo wa nje, na si wa kwetu hapa nyumbani?

Naomba nieleweke vyema. Kikwete kama mtu binafsi ana uhuru wa kumshabikia Ronaldo na Real Madrid au mwanamichezo yoyote yule, lakini kama rais; si vyema kufanya hivyo hadharani, na tena katika hafla rasmi za Ikulu.

Kwa maana hiyo, ningemuelewa vyema Kikwete kama angekuwa anamshabikia Ronaldo kimya kimya sebuleni kwake.

Ningemuelewa kama angeipokea jezi hiyo kimya kimya sebuleni, na pengine kuigawa hapo hapo. Lakini kwa kulifanya tukio hilo kuwa ni rasmi; kiasi hata cha kuita wapiga picha; maana yake ni kwamba analithamini, analirasimisha na analipa kipaumbele!

Kinachogomba hapa ni pale anapoitumia Ikulu na urais kumshabikia mwanasoka wa nje - Ronaldo. Usisahau kwamba huyu ni rais wa nchi, na kila alifanyalo katika hafla rasmi inayofanyika Ikulu, anakuwa ni kioo cha Taifa – kioo cha uzalendo wetu sote ndani na nje ya nchi.

Inapotokea Rais mwenyewe anamshabikia Ronaldo hadi kwenye hafla rasmi ya Ikulu, ni dhahiri wajibu huo wa kuwa kioo cha uzalendo wetu sote ndani na nje ya nchi unadhoofika.

Labda ni kwa sababu ya hulka hizo za watawala wetu za kupapatikia vya nje, hatupaswi kushangaa kuiona televisheni yetu ya taifa (TBC) ikionyesha ‘live’ mechi za Ligi Kuu ya Uingereza, lakini haifanyi hivyo kwa mechi za Ligi Kuu yetu ya hapa nyumbani. Kuna uzalendo gani tunaweza kuujenga kwa kuonyesha ‘live’ ligi ya nje badala ya ligi ya nchi yetu wenyewe?

Aidha, kwa kitendo kile cha Kikwete cha kupigwa picha Ikulu akipokea jezi Na. 9 ya Ronaldo, na picha hiyo kuchapishwa na magazeti na kuingizwa kwenye tovuti mbalimbali duniani, Rais Kikwete ametumika kutangaza, kote duniani, biashara ya Real Madrid ya kuuza jezi Na. 9 ya Ronaldo! Kwa maneno mengine, ni endorsement ya bure kabisa ya kibiashara ya Rais wetu kwa jezi namba 9 ya Ronaldo!

Sasa hapo ni uzalendo gani aliouonyesha Kikwete kwa Watanzania kwa kukubali ‘zawadi’ ya jezi ya mwanasoka huyo wa kigeni? Hata kama amefanya hivyo ili eti kuishawishi Real Madrid ije nchini, sote tunajua kwamba timu hiyo haina “udugu” na nchi yoyote duniani, na kwamba inachojali ni kutengeneza mapesa tu. Itakuja nchini kama italipwa mapesa inayotaka, na itakwenda hata Bermuda kama ikilipwa mapesa inayotaka.

Kwa mtazamo wangu, hali ingekuwa ni tofauti kama jezi aliyoipokea Kikwete, Ikulu, ingekuwa ni ya yule Mtanzania mwenzetu anayeng’ara nchini Marekani katika ligi ya mpira wa kikapu ya NBA, Hasheem Thabeet. Hapo, uzalendo ungekuwepo, na hata uhalali wa kuvaa T.Shirt yake ungekuwepo.

Ni kwa msingi huo naelewa ni kwa nini Watanzania wengi wanaoishi Uingereza ndiyo walionitumia e-mails za kuonyesha kukerwa na suala hilo la Kikwete na jezi ya Ronaldo. Walikiona kitendo hicho kuwa hakichochei Watanzania kujenga utaifa na uzalendo kwa taifa lao, kwa sababu hakitangazi u-Tanzania.

Nawafahamu baadhi ya Watanzania hao. Baadhi yao ni wale wanaodiriki kusafiri kilomita nyingi, jijini London, mwishoni mwa wiki, kufuata baa ya Mhindi mmoja inayouza bia aina ya Serengeti. Watanzania wale hujisikia raha mno wanapokunywa bia ya nyumbani Tanzania katika baa ya London iliyojaa Wazungu - bia yenye chupa iliyoandikwa “brewed in Tanzania”!

Naamini ni uzalendo tu ndiyo unaowatuma kufanya hivyo ugenini, na kama ndivyo, basi, lazima uielewe hasira yao wanapoona picha ya rais wao akikabidhiwa jezi za mchezaji wa kizungu wa Ulaya, na si jezi ya Mtanzania mwenzao, Hasheem Thabeet! Si ilisemwa ya kwamba: Mcheza kwao hutuzwa?

Tukirejea kwa ya Mkapa; ya kwake hayana hata mjadala mkubwa. Huwezi kuwathamini waandishi wa nje na kuwapuuza wa nchini mwako, na kisha ukajitia wewe ni mzalendo.

Huwezi kukaa Ikulu, kwa miaka 10, kama rais wa nchi na usifanye lolote kujenga uzalendo, na kisha unapotoka Ikulu ndipo ulalame kwamba tatizo letu kubwa ni kukosa uzalendo! Alifanya nini kujenga uzalendo alipokuwa rais?

Huwezi kukaa Ikulu kwa miaka 10 na kuongoza serikali iliyogubikwa na ufisadi wa kila aina (EPA, Meremeta, Deep Green nk); huku mwenyewe ukituhumiwa kununua kampuni ya umma (Kiwira) kwa bei ya kutupa, na kisha ukitoka Ikulu ulalame kwamba hakuna ‘uzalendo’ nchini! Ni uzalendo gani anaomaanisha Mkapa?

Kama hata waandishi wenyewe wa Tanzania hawapendi, na anaowapenda ni wa Ughaibuni, angewezaje kuujenga huo uzalendo kwa Watanzania wakati wa kipindi chake cha urais?

Isitoshe, hivi Mkapa hajui kwamba ni vigumu mno kujenga uzalendo katika nchi ambayo imegawanyika katika matabaka mawili makuu ya walichonacho na wasichonacho?

Hivi katika mazingira yetu hapa Tanzania; mtoto wa mkulima masikini na mtoto wa mfanyabiashara tajiri wanaweza kweli wakachangia maana ile ile ya uzalendo? Nina shaka.

Hivi Mkapa hajui kwamba tafsiri ya neno ‘mzalendo’ inazidi kupoteza maana yake hapa Tanzania; kiasi tunavyojenga jamii isiyo na haki, jamii ambayo wachache hufaidika vilivyo na keki ya taifa; huku walio wengi wakiogelea katika lindi la umasikini?

Hivi Kalimanzira na Patel Khulibhai wanaweza kweli kuchangia tafsiri moja na maana ile ile ya neno ‘mzalendo’? Nina shaka.

Ndugu zangu, ni kweli tuna tatizo la ukosefu wa uzalendo, lakini viongozi wetu hawa wa zama hizi hawawezi kukwepa lawama za kuhusika na kuongezeka kwa tatizo hilo. Viongozi wanapotumia nafasi zao za uongozi kujitajirisha, kamwe hawawezi kuwa na utashi wa kuujenga uzalendo.

Nihitimishe kwa kusisitiza kwamba uzalendo hushamiri tu kwenye nchi yenye misingi ya haki na inayotoa fursa sawa kwa wote. Kwa maana hiyo, uzalendo utazidi kuota mbawa nchini; kiasi tunavyozidi kupanua wigo wa walichonacho na wasichonacho, na kiasi watawala wetu wanavyozidi kuwapendelea wale walichonacho na kuwatelekeza wanyonge.

.

No comments:

Post a Comment