Tuesday, March 2, 2010

KIMBUNGA CHA XYNTHIA KIMEUA 56 BARANI ULAYA


Watu 56 wameuawa katika kimbunga kilichopiga siku ya Jumapili magharibi ya Ulaya. Upepo uliofikia mwendo wa kilomoita 175 kwa saa umengóa miti na minara ya umeme na kusababisha watu kukaa gizani.

Kimbunga hicho kilichoitwa Xynthia kilitokea Bahari ya Atlantik na kikapiga katika pwani ya magharibi ya Ufaransa na Uhispania kabla ya kuendelea hadi Ureno, Uholanzi na Ujerumani.

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy hii leo anatembelea eneo la pwani lililoathirika vibaya zaidi. Kimbunga kilichofikia mwendo wa kilomita 175 kwa saa na mawimbi ya urefu wa mita nane yamesababisha mafuriko hadi katika maeneo ya ndani na watu walipaswa kukimbilia kwenye mapaa ya nyumba.
Dhoruba hiyo imeng'oa miti na minara ya umeme, na mamilioni ya watu wamebakia bila ya umeme hasa katika eneo la pwani la Brittany. Kwa mujibu wa shirika la umeme la Ufaransa EDF, hali hiyo huenda ikaendelea kwa siku kadhaa. Hata misafara ya ndege na treni imevurugwa na maelfu ya abiria walinasa katika stesheni za treni na kwenye viwanja vya ndege.

Waziri Mkuu wa Ufaransa, Francois Fillon amesema, atatangaza kimbunga hicho kuwa ni maafa ya kimaumbile na kutatolewa fedha maalum kusaidia kazi za ukarabati katika jamii. Ufaransa itawasilisha maombi yake katika Umoja wa Ulaya kupatiwa fedha hizo kutoka fuko maalum ili kusaidia operesheni za ukarabati. Nchini Ufaransa pekee imethibitishwa kuwa watu 47 wameuawa na wengine 30 hawajulikani walipo.

Kimbunga Xynthia kilifika Ujerumani,Ubeligiji na Uholanzi Jumapili mchana na kikaendelea kuvuma hadi usiku na kuvuruga misafara ya treni na ndege. Huku Ujerumani watu wawili walipoteza maisha yao baada ya kuangukiwa na miti. Na Uhispania pia wanaume wawili waliokuwa katika gari waliuawa walipoangukiwa na mti na nchini humo humo mwanamke mmoja mzee alifariki baada ya kuangukiwa na ukuta.

Nchini Ujerumani, shirika la treni Deutsche Bahn jana jioni lililazimika kufuta safari nyingi kwa sababu ya miti iliyoangukia njia za reli. Waokozi wamefanya kazi usiku mzima kuhakikisha shughuli za usafiri zinaanza kufanya kazi. Kimbunga Xynthia sasa kinaelekea kaskazini ya Ulaya.

No comments:

Post a Comment