Monday, March 1, 2010

WAARABU NA UKATILI DHIDI YA VIJANA WA KIKENYA

Ukosefu au upungufu wa rasilimali ya kutosheleza mahitaji ya mwanadamu ndio chanzo kikubwa cha watu kuhangaika huku na kule na hata mara nyimgi kuhamia katika mataifa ya kigeni, hali hii inachangiwa zaidi na ongezeko la kiwango cha uasikini, mfano barani Afrika ambako idadi ya wahamiaji wanaotafuta maisha bora katika mataifa ya kigeni inazidi kuongezeka kila uchao.
Lakini si wengi wanaobahatika au kufaidika na uhamiaji huo,uwe wa halali au kinyume, na mwishoe wahamiaji hawa hujikuta katika utumwa mamboleo ndio mada tunayozungumzia hii leo, na jinsi haki za wahamiaji hawa zinavyoendelea kukanyagwa na wabepari wanao ahidi pepo,hasa katika mataifa ya kiarabu.
Idadi ya wasichana kwa wavulana wanaohamia katika mataifa ya kiarabu kutafuta ajira imekua ikiongezeka kwa kasi mno nchini Kenya katika siku za hivi punde, Vijana wengi walekua wakikusanyika katika ofisi za makampuni na mashirika ambayo yamejitwika jukumu la kuwa mawakala wa kuwatafutia ajira vijana hawa katika mataifa ya eneo la Mashariki ya kati.
Kwa wengi hii huwa fursa muafaka na rahisi ya kuupiga teke umasikini, mbali na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini kenya, vijana hawa hulazimika kulipa kiasi kikubwa cha pesa ili kupata nafasi ya kwenda kufanya kazi katika mataifa haya ya kiarabu, kwa kuzingatia hali ya umasikini unaokithiri, vijana hawa hufanya kila juhudi angalau kupata pesa za kulipa ada hio.
Lakini kinachosikitisha zaidi ni kwamba si wengi wanaobahatika kusafiri na baadhi yao huangukia mikononi mwa mawakala walaghai ambao hutoweka na pesa hizo. Mzee Ngarib Chuba ni miongoni mwa watu ambao waeekumbwa na kadhia hiona alikutwa katika moja ya ofisi za wakalahuko Kenya, na alipofanya mazungumzo na mwandishi wa habari alisema,
"Ilitangaza kwa maredio kwamba kuna kazi Dubai na wakaambiwa watasafiri baada ya wiki mbili mimi mwenyewe nio na watoto watatu, mmoja nilimuachisha kazi nikaja nae hapa ili apate safari lakini hatimae hakuna safari"
Kijana mwengine ambae jina lake halikupatikana mara moja alisikika akisema "sisi tumeuza vitu vya nyumbani maredio ma tv kila kitu".
Kwa kawaida watu wanaotaka kusafiri au kutafutiwa ajira katika mataifa haya ya kiarabu, hulazimika kulipa ada ndogo kati ya elfu kumi na tato ( Sh 15,000) hadi shilingi elfu ishirini na tano ( 25,000) pesa za Kenya sawa na dola mia mbili hadi mia tatu ( $ 200-300) za Kimarekani.
Lakini kwa bia Aisha Sharif Nuur mkaazi wa Mtwapa yeye kwake mambo ni tofauti, kwa upande wake yeye alifanikiwa kusafiri hadi nchini Saudia safari iliyotarajiwa kuleta mengi mzruzi kwa familia nzima hivyo ilikua ni vigere gere kwa familia hio, kwani njia ya kupiga teke umasikini ilionekana ni yenye kufunguka, na hata watoto wake wawili Omar na Leila wakawa na matumaini ya kukamilisha masoo yao baada ya kuacha skuli kutokana na kushindwa kulipa ada.
Punde tu alipowasili katika uwanja wa ndege nchini Saudia ulimwengu ulimgeukia bi Aisha na matumaini yote aliyokua nayo yakaanza kudidimia.
"Walitwambiaaa...huyo agent wa Nairobi ndio alitwambia mtalipwa mia nane ya kule kwahio ni shilingi 16,000 ya Kenya, kufika airport ua sauida tulikaa siku tatu kufika siku ya tatu ndio akaja huyo mwarabu ndio aliniandika kazi, kuingia ndani ya gari akanambia nimpe paspoti, akachukua paspoti ndio basi" alisema bi Aisha.
Mzingira ya watu wakatili wasiojali utu seuze mshahara kwa kazi ambayo hadi kuwasili kwake mjini Jiddah hakua amefahamishwa kazi anayokwenda kufanya "kazi zao ni 24/7 hakuna kulala, unarauka saa kumi na moja alfajiri mpaka saa nane ya usiku, wenyewe wanakuita fanya hivi fanya hivi, sugua hapa sugua hapa, chakula wanakula kuku mzima na mchele wanafunga na mfuko hivi wa plastiki tena sasa haya wanaanza kuminyana tena hapo, ukila ukikata hivi nyama ndani mbichi, hizi chupa kubwa za mineral unakata juu ndio unafanya jagi ya kwenda kutekea ile chai" aliongeza bi Aisha.
Bi Aisha anasema kua wasichana hawa punde tu wanapowasili kwa matajiri wao wapya huwa ni sawa na kuuaga uhuru wao mbali na kufanyishwa kazi ngumu isiyo na mshahara,
sawa na utumwa.
"Tulipelekwa tukapigwa picha tukaandikwa majina kwa kiarabu, nje ulikua hutoki wenyewe wakitoka tu hata kama wanakwenda msikitini wanafunga mlango sasa siwezi toka, halafu mahali pa kulala sikupata mahali pazuri, wananiweka tu hivi seating room akija yule mama anakukanyaga kanyaga tu hivi, huwa nalala chini pia natumia dawa mimi za alsa huwa namwambia ninunulie dawa basi yuanambia ni mrongo, nikaenda kwa jirani hapo mbele nikabisha, huyo jirani nikamwambia nisaidie mimi ni mgonjwa akanambia nikikusaidia utaniletea shida wewe vile ni Mkenya"alilalamika bi Aisha.
Biashara ya ulanguzi ya binaadam ni dhahiri licha ya mataifa ya ulimwengu kufokea biashara hii, na hapa tena bi Aisha nuur bado anaendelea kuelezea mkasa ulimkumba akiwa Saudia "huyo mwarabu alietuchukua Nairobi alituchukua kama sisi watumwa, waona vile alinambia ataka laki mbili manaake alituuza sisi laki mbili kwa yule Msuudia, alipewa laki mbili sasa ametufanya kama watumwa anatuuza,kwa hio alinambia kama wataka kurudi unipe laki mbili tumrudishie yule mwenyewe, nio ndani jela huyo mwaabu anambia mimi wataka kurudi Kenya? mpaka unitumie dola elfu mbili ndo urudi Kenya, nikamwambia hio dola elfu mbili mimi nitaitoa wapi?".
Lakini bi Aisha hayuko peke yake, raia wengi wa kigeni hasa kutoka Ufilipino, Nigeria n.k, wanaendelea kuteseka mikononi mwa makatili hao na huenda wasionekane tena na jamaa zao.
Lakini kwa nini iwe hivyo? au Serikali ya Saudia imelipa kisogo suala la haki za binaadam?.
"Kusema lile la kweli ma Argent nao hawana uzalendo wanahaja na pesa, hawajali utaenda wapi utakutana na nani utalala wapi utaishi vipi , yeye bora ile comission yake ameipata kutoka kwako na kutoka kwa mwenye ambae anaenda kukuajiri basi kwake siku imepita"alisema mtu mmoja ambae hakujuilikana jina lake.
Huko nchini Kenya pekee, duru zinaeleza kwamba mamia kwa maelfu ya wasichana wadogo wanaendelea kuteseka katika nyumba za matajiri makatili nchini Saudi Arabia baada ya pasi zao kuzuiliwa ili waendelee kufanya kazi ngumu nchini humo.
Bi Aisha yeye alikua na bahati japo baada ya kuteseka kwa muda na kuhangaishwa kutoka gereza moja hadi jengine, hatimae msamaria mwema ambae ni mwenyekiti wa shirika la Kiislam la ustawi wa vijana mjini Mombasa Khalid Jiraini aliweza kumsaidia kukimbia ukatili huo Nchini Saudia.
Khalid anasema kwamba inasikitisha kuona kwamba serikali inavyoshuhulikia suala hili na kuongeza kwamba tayari shirika lake limewasilisha malalamishi kwa serikali ya Sauida kuhusiana na suala hilo.
Sasa bi Aisha anafurahi kurejea nyumbani salama wa salmin japo bila ya hati yake ya usafiri wala mshahara mkubwa alio ahidiwa, huku akiendelea kuwaombea wenzake aliosafiri nao hadi Saudia ambao hajawahi kuwaona tena tangu kuwasili katika uwanja wa ndege wa Jiddah.
Serikali ya Kenya haijatoa tamko lolote kuhusiana na suala hilo licha ya visa vingi kuangaziwa kuhusu wakenya ambao wanaendelea kuteseka katika mataifa ya kiarabu.

No comments:

Post a Comment