Thursday, March 11, 2010

Wanaharakati alfu 5 waandamana Nigeria


Kiasi cha wanaharakati alfu 5 wameandamana hii leo ili kulishinikiza baraza la mawaziri kujiuzulu pamoja na kumtaka Rais Umar Yar'Adua anayeugua awahutubie wananchi.Ni wiki mbili tangu kiongozi huyo arejee nchini baada ya kutibiwa nchini Saudi Arabia.


Maafisa wa polisi waliwasimamisha waandamanaji hao walioongozwa na mchungaji maarufu wa Lagos Tunde Bakare walipofika karibu na makazi ya rais walikopanga kumuwasilisha madai yao Kaimu Rais Goodluck Jonathan.

Madai hayo yalipokelewa-kwa niaba ya Kaimu Rais- na katibu wa serikali ya shirikisho Yayale Ahmed. Wanaharakati hao wanalitaka baraza la mawaziri lijiuzulu kwa sababu lina mitazamo inayogongana kuhusu suala la afya ya Rais Yar'Adua.

Waandamanaji hao waliozuiliwa kuingia bungeni walidai pia kuwa wanaitaka ripoti ya kamati ya bunge kuhusu mageuzi ya sheria za uchaguzi itekelezwe. Wanaharakati hao wameandamana pia katika miji ya Abuja, Lagos na Benin mwaka huu.

Wakati huohuo kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa serikali, idadi ya waliouawa katika mapigano ya Jos imepungua hadi 109 na watu 49 watashtakiwa kwa kuzisababisha ghasia hizo. Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Benedict wa XVI ameyalaani mauaji hayo yaliyotokea siku ya Jumapili.

No comments:

Post a Comment