Wednesday, March 10, 2010

MAALIM SEIF HAJATOKA SPITALI


Afya ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, inaendelea vizuri ingawa hajaruhusiwa kutoka hospitali kama alivyotarajia.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Maalim Seif aliugua ghafla akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, akisubiri ndege kuelekea Oman kwa shughuli binafsi.

Hata hivyo, ugonjwa wa katibu mkuu huyo ulizua hofu ya kifo miongoni mwa Watanzania baada ya ujumbe kuhusu uzushi wa kifo cha kiongozi huyo mkongwe wa kambi ya upinzani kuenezwa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za kiganjani huku wengine wakidai kuwa amelishwa sumu.

Katika kuthibitisha hayo, gazeti hili juzi lilifika katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini, alikolazwa Maalim Seif na kuzungumza naye ambapo alikiri kuugua ghafla maradhi ya kupanda kwa shinikizo la damu ingawa anaendelea vema.

Maalim Seif alisisitiza kwamba hali yake ipo vema na madaktari wanajitahidi kuhakikisha shinikizo la damu linalomsumbua tangu mwaka 1989 linadhibitiwa ili aweze kuendelea na shughuli zake za kisiasa kama kawaida.

Hata hivyo, kiongozi huyo anayetarajia kuwania urais wa Zanzibar aliwashukuri wananchi wote walioguswa na ugonjwa wake na wanaomwombea apone haraka huku akiamini kwamba angeruhusiwa kutoka hospitalini hapo jana.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, wa chama hicho chenye makao yake makuu Buguruni, Dar es Salaam, Salim Bimani, alisema bado Maalim Seif yupo hospitalini kwa uangalizi zaidi.

“Maalim bado yupo hospitalini kutokana na ushauri wa daktari wake ila anaendelea vizuri... nadhani ni kwa sababu ya kumpa mapumziko marefu huku wakichunguza afya yake kila wakati.

“Tunaamini katika siku mbili hizi ataruhusiwa kwa sababu presha yake imerudi kwenye hali ya kawaida, lakini lazima tufuate ushauri wa daktari,” alisema Bimani.

No comments:

Post a Comment