Tuesday, March 9, 2010

WAMOMBASA NA HARAKATI ZA UKOMBOZI WA NCHI YAO

Historia inaandika kwamba, ukanda wa Pwani ambao ulikua chini ya Sultan Said Bin Ali Bin Said wa Oman, haukua chini ya utawala wa Uingereza wakati wa ukoloni, wenyeji wake ambao ni wa miji kenda yaani makabila tisa yaliyoungana bado wanaamini kua ukanda huu wa pwani, si sehemu ya Jamuhuri ya Kenya kwani mpaka wake uko katika eneo la Sultan Hamoud nje kidogo tu ya mkoa wa Nairobi.

Eneo la Sultan Hamoud ndipo kituo cha mwisho cha Sultan huyo wa Oman alipoweka majeshi yake baada ya kuwafurusha wavamizi wa Kireno kutoka katika ukanda wa Pwani na kutangaza himaya yake kunako karne ya kumi na sita.

Randu Nzae Ruwa ni mwana historia na katibu wa vugu vugu la Repablican Concil of Mombasa, linalo tetea uhuru wa jimbo hili anaeleza kuhusu ukanda huu wa Pwani.

"Pwani haijatawaliwa, Pwani katika Serikali zote zinanokuja hapa huwa zinakuja na mikataba, kama ni mreno aliingia hapa Pwani na mikataba, yeye alikua shughuli zake ni za baharini pamoja na kuuwa ndovu akichukua pembe akipeleka kwao, ikawa anawa treat vibaya wa Pwani ndipo Wapwani wenyewe 1661 wazee wa Pwani wakafanya safari mpaka Oman, na mwarabu alipokuja hapa akampiga kweli Mreno na akaondoka katika nchi yake kutoka baharini mpaka Sultan Hamoud akamkatisha kipande na akampatia rahani Sultan.

Malikia alipokuja akitaka atumie kipande cha bahari na yeye, wazee wa Pwani wakazungumza pale 1895 ukaandikwa mkataba tarehe 14 juni, wakaja wakakaa tena wakaandika tena mkataba mwengine tarehe 14 Disemba 1895 na yale mambo ambayo Serikali ya Uingereza ilikua itafanya hapa".

Hii ndio maana wenyeji wake mara kwa mara wamekua wakijitokeza kubuni makundi ya kudai uhuru wa jimbo hili hasa wanapohisi kukandamizwa zaidi na Serikali kuu Nchini Kenya, hali hii inathibitishwa na sera na siasa za Wapwani ambao miaka nenda miaka rudi wamekua wakipibania serikali ya majimbo nchini Kenya, na hapa tena Randu Ruwa anelezea.

"Pwani na Kenya ni Nchi mbili tofauti ambazo ziliwekeana mkataba, na mkataba huu uliandikwa tarehe 8 Octoba mwaka 63 na aliekua British High Commssioner Sir Jems Robertson, ndio akasema kwamba Wapwani sasa hivi wasijitawale wenyewe watawaleni kimajimbo na Kenya na wakitaka uhuru wao wapewe uhuru wao wenyewe, lakini baada ya hio katika ya Lancasterte House ukaandikwa tena mkataba huko huko Lancaster House kwamba serikali ya Kenya itaingilia majukumu kuhusiana na ulinzi, akawapatia tena miaka 50 ya uhuru, baada ya miaka 50 ya uhuru ndio warudi tena waka declare, kama kutakua hakujatokezea Wapwani waksema wanaonewa na Wakenya basi itabidi iwe Kenya ni moja, lakini wakisema wanaonewa itabidi itabidi hizi Nchi zigawanywe ziwe mbili, ambapo ambapo miaka 50 ya uhuru ni 2013".

Mkoa huo wa Pwani unafahamika kwa mchango wake kiunchumi kwa Taifa zima la Kenya, ni hapa kunakokutanika bandari kubwa kabisa inayojuilikana kama ni mlango wa eneo zima la Afrika Mashariki na kati.

Mbali na hayo, ukanda wa Pwani una ardhi kubwa yenye rutuba na rasili mali za kila aina, lakini kwa wenyeji hawa rasili mali hizi azijamfaidisha Mpwani tangu pale Kenya ilipojinyakulia uhuru huku wakiendelea kukandamizwa na hata kunyang'anywa ardi zao na wageni kutoka sehemu nyengine za Jamuhuri, kama anavyosimulia mwanachi mmoja wa Pwani.

"Tumenyanyaswa katika ardhi zetu, kama mimi mzee ambae nimefikia karibu umri wa miaka 60, bado sina tittle ya pwani, naitwa ni escorter na kama ni escorters tunamu escort nani?, jambo la pili rasilimali za Pwani ambazo zinatoka katika hili jimbo la pwani huwa baadae yote inaenda katika headquarters, sisi ilikua turudishiwe kam 60% lakini tunarudishiwa 2% ambapo haiwezi ku develop mambo ya Pwani".

Hichi ndicho chanzo cha kuzuka kwa mapigano makali katika kusini ya mji wa Mombasa, mapigano ambayo yalifahamika kama Kayabombo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1997 ambpo watu kadhaa wakiwemo viongozi wakuu wa vugu vugu hilo waliuawa.

Lengo kuu la kuzuka kwa mapigano hayo ilikua ni kuwafurusha wageni waliovamia ardhi inayodaiwa kuwa ni ya Mpwani.

Sasa vugu vugu au chama cha Republican Concil of Mombasa (RCM) kiko katika mstari wa mbele baada ya kujitwika jukumu la kulikomboa eneo hili la Pwani nzima na tayari limetoa makataa kwa Serikali ya Muungano nchini Kenya.

Nae katibu wa chama hicho bwana Randu Ruwa, alipoulizwa juu ya kuundwa kwa chama hicho katika kipindi hichi ambacho Serikali ya Kenya iko mbioni kuunda katiba mpya itakayojumuisha Serikali za majimbo, nae alikua na haya ya kusema.

"Katiba ambayo inatayarishwa saa hii sisi hatutaki iwaguse Wapwani, hio na iwe ni ya Kenya na iwe ni Doccument ya Kenya, wale wa Pwani wasiwe ndani, mwezi wa kumi na moja tulimuandikia barua Mh Rais Kibaki tulimuelzea sisi Wapwani saa hii hatuna haja tena na mambo ya Kenya, na kopi yake tumepelekea Malkia, na kopi hio hio tumepeleka kwa Bunge la East Afrika, na kopi hio hio pia tumepelekea kila mbunge wa Pwani, pia kuna kopi hivi iko njiani inaenda kwa Sultan wa Oman".

Baraza hili lina vitengo vitatu, ikiwa ni pamoja na kitengo cha baraza la Utawala, baraza la Vijana na baraza la Wazee kutoka jamii ya miji kenda kwa jina maarufu wazee wa Kaya, na hapa ni Juma Rashi Gasare Mwenyekiti wa baraza la wazee wa miji kenda tawi la Miritini Mjini Mombasa.

"Hawa vijana walikua wakiitwa ni wakora na Serikali ya Kenya, mara wanaitwa wao ni wauaji, sasa sikuweza kuwaelewa, tulipowaita walikuja na kutuelezea zile sera zao kwamba wao lengo lao ni kutaka kukomboa hii Pwani kutoka katika mikono ya Serikali ya Kenya, kwa sababu walituonesha makubaliano yale yaliyoandikwa mbeleni kutoka katika utawala wa zamani na sisi tukaona hawa vijana ni wakweli".

Lakini ni jukumu gani linalotekelezwa na baraz ahili la wazee?, hapa tena Mzee Gasare anaeleza zaidi.

"Tuliwaunga mkono ili tujaribu kuwasaidia kuhamasisha wale wenzetu ambao hawajaelewa maana ya hichi chama, niliiomba Serikali isijaribu kutumia silaha, ikiwa ni mikataba kubadilishwa basi wakae chini kubadilisha mikataba kwa njia ya amani bila ya umwagaji damu".

Lakini hatua hii haijapokelewa vyema na Serikali ya Kenya inayolitaja kundi hili kua ni kundi la kigaidi linalotaka kuzua machafuko katika eneo zima la Pwani.

Mnamo mwaka wa 2005 wafuasi watano wa kundi hili la Republican Concil of Mombasa, waliuawa katika msitu wa Mlungu nipa unaopatikana kusini mwa mji wa Mombasa, baada ya maafisa wa usalama kuwafumania wafuasi wake katika eneo la ibada, wakidai kua ni wafuasi wa kundi haramu linalojihusisha na vitendo vya ugaidi na kula kiapo kuzusha ghasia mjini Mombasa.

Utawala wa Mkoa kupitia mkuu wa mkoa Ernest Mwinyi umepuuzilia mbali baraza hilo na kutangaza msako mkali dhidi ya viongozi wake, dai linalopingwa vikali na baraza hilo, kama anavyoeleza mzee Rashid Gasare.

"Hawa si wakora kwa sababu kama ni wakora hawange andikia Prime Minister barua, hawangepeleka barua kwa Mwai Kibaki, hawangepeleka barua kwa Malkia Elizabeth wa London, wanakiita ni kikundi ni haram lakini wenyewe ni wazaliwa wa hapa kwa hivyo wenyewe kama si haramu kwa nini kikundi kiwe haramu?".

Hivi sasa shirika hilo limo mbioni kuchangisha pesa za na kusafiri hadi Uingereza kwa madhumuni ya kukutana na Malkia wa Uingereza katika juhudi za kusukuma agenda yao.

No comments:

Post a Comment