Tuesday, March 9, 2010

UMEME WAREJEA UNGUJA, WATU WASHEREHEKEA KWA KUSEMA: EID EL UMEME

Wenyeji kisiwani Unguja wamepata afuweni ya kurejeshwa nishati ya umeme baada ya miezi mitatu ya kukaa kwenye giza, na wakati wenyeji ndio wanasubiri kuona ikiwa ndio mwisho wa athari walizokumbana nazo kufuatia bidhaa hio kutoweka kwa muda mrefu, mwandishi kutoka Zanzibar Ali Saleh ana taarifa juu ya hili.

Kama ambavyo Shirika la umeme Zanzibar lilivyokua liksema kua jana wakati wa saa tisa mchana kua umeme utarudishwa, kwa njia ya majaribio na AlhamduliLlaah hilo likawa, lakini hii ni baada ya ahadi nyengne mbili kushindwa kutimizwa.

Kwanza Serikali ilikua imeahidi umeme ungalirudi Zanzibar mnamo Febuari 20 baada ya kuondoka siku ya Disemba 10 mwaka jana lakini hilo halikuwezekana na kusogezwa hadi Febuari 28, na tarehe hio nayo ikapita bila ya mafanikio na ndipo tarehe mpya ikawa ni ya jana na leo ndio umeme unatarajiwa kurudi rasmin hapa Unguja.

Kuzimika kwa umeme kulitokana na kutokea maharibiko katika kituo cha kupokelea umeme cha Fumba na kuhitajika utaalamu mkubwa kiasi ambacho mafundi kutoka Afrika Kusini na Bara Ulaya wakahitajika na hapana shaka mamilioni ya fedha kutumika.

Ukosefu wa umeme umesababisha uhaba mkubwa wa maji, na ingawa Serikali ilitumia kiasi kikubwa cha fedha kusambaza huduma hio lakini haikufua dafu, na mahitaji yakawa makubwa kuliko uwezo.

Uchumi wa visiwa hivi utakua umepata pigo wakati ambapo Shirika la umeme peke yake litakua limepoteza mapato ya Shilingi bilioni tano na nusu, na hapana uchumi huo wa Zanzibar unaotegemea huduma kama vile mahoteli utakua umepata pigo litakalochukua muda mrefu kuunga.

Mahoteli kadhaa yalipunguza huduma zake na wafanya kazi kupunguzwa na huku huduma za Kiserikali zikafanywa chini mno ya hali halisi na bidhaa kadhaa zikapanda bei kwa vile zilihitaji gharama kubwa ya kulipia petroli au dizeli.

Wakosoaji wameilamumu Serikali ya Zanzibar kwa kukosa umakini wa kutolipa uzito suala hilo la umeme hata baada ya umeme kukatika kwa mwezi mzima hapo mwaka 2008 na bila ya kua na utaratibu mbadala kama vile majenereta ya dharuraambalo jambo ambalo serikali halitaki litokee tena kwa vile sasa hivi linakamilisha taratibu za kuwa na umeme wa dharura iwapo hali kama hio itatokezea tena.

Umeme umerudi hapa Unguja lakini bado kuna mashaka juu ya uwezo wake wa kudumu kwa vile waya wake unaopita chini ya bahari kutokea Tanzania bara ni mkongwe mmno, lakini tukitaraji itakua salama hadi utakapokamilika mradi mwengine mkubwa wa umeme unaolipiwa na Serikali ya Marekani, ambao pia utapitia chini ya bahari.

Lakini hayo ni matarajio tu na matarajio ni ya mjaaliwae, kwa sasa umeme wa Unguja ambao uliwahi kupewa jina la kivunge, usije ukapulizwa na ukazimika, ingawa kwa sasa hapa nilipo namurikwa na umeme na kupepewa na feni ambalo sijaliona kwa miezi mitatu hivi sasa.

No comments:

Post a Comment