Sunday, March 14, 2010

TOBA INAHITAJIKA

Nimekaa na kutafakari juu ya haya majanga yanayoikumba Zanzibar kila baada ya muda ni kwa sababu gani au kwa nini. Hatuendi mbele kimaendeleo na wala hatupo pale pale bali tunazidi kurudi nyuma. Tukiangalia hatuna maendeleo kwa maana ya maendeleo,
kwa hili halina ubishi.

Sitaji udhaifu wa sekta za Serikali moja baada ya nyengine kwa vile sisi wenyewe [Wazanzibari] tunajua ukweli na hali halisi ya sekta hizo.

SMZ ingelikuwa hoi bin taabani kama kungelikuwa hakuna huduma binafsi kama vile maskuli, mahospitali na hata usafiri kama vile daladala, meli na ndege, wao wangezimudu vipi huduma hizi peke yao ?

Maafa ya meli kuzama, maafa ya kukosa umeme kwa miezi mitatu, maafa ya kukosa maji wakati chemu chemu ipo na hili la mwisho la kuungua Serengeti, inafaa tujiulize 'kwa nini sisi tu ?'

Mapinduzi ni jambo la kawaida la kubadilisha serikali popote pale ulimwenguni, kuna ya mauaji na kuna yale baridi [palace revolution], na hapa nazungumzia yaliotendeka na sio mapinduzi yenyewe. Kwa upande wetu na kwa mujibu wa mambo yalivyokwenda bila ya shaka ipo haja kubwa ya kutubia kwa Allah Subhana Wa Taala ili atusamehe kwa maovu yaliotokea 1964 ikiwa ni wakati wa mapinduzi yenyewe au baada ya mapinduzi.

Inawezekana kukusanyika tena pale pale Maisara na kumuomba Allah atusamehe kwa maovu hayo yaliotendeka ili nchi yetu Zanzibar ifunguke na kuingia neema badala ya nakama, kwa hili hakuna kuona haya na wala aibu, kama watu walivyokusanyika kwa kuombea dua maridhiano yaliyofikiwa baina ya Maalim Seif na Rais Karume. Innallaha Ghafurun Rahiym ijapokuwa Shadidul Iqab. Mara zote binadamu lazima arejee kwa Muumba wake.

A.N.

No comments:

Post a Comment