Sunday, March 14, 2010

TATIZO LA UMEME ZANZIBAR LITUPE FUNZO

UNYONGE mkubwa uliowakumba watu wa kisiwa cha Unguja kwa kukosa huduma ya umeme kwa miezi mitatu limemalizika.watu hao walikumbwa na zahama hiyo kwa sababu ya kukatika ghafla kwa huduma hii ya nishati baada ya mtandao wa kuleta umeme kisiwani kwa kutumia waya uliotandikwa chini ya Bahari ya Hindi kuoka Bara kuja Unguja kuharibika vibaya sana tarehe 9, Desemba, mwaka jana.

Hata hivyo, wananchi katika baadhi ya maeneo ya mjini, kaskazini na kusini Unguja bado wanaendelea kusubiri kupata huduma hii muhimu kwa maisha ya kila siku kutokana na sababu mbali mbali. Hii ni pamoja na kuelezwa kuwepo kwa hitilafu za kiufundi na kuibiwa nyaya za umeme na mafuta katika transfoma zinzosambaza umeme katika sehemu hizo.

Kukosekana kwa umeme kwa kipindi cha miezi mitatu kumetoa mafunzo mengi kwa serikali, taasisi mbali mbali na mwananchi wa kawaida . Kuyadharau mafunzo yaliyopatikana ni kujitafutia hatari na shida kubwa zaidi siku za usoni.

Miaka miwili iliyopita mfumo huu wa kuleta umeme kutoka Bara ulikatika ghafla na ilichukua mwezi mmoja kwa huduma kurejea kama kawaida.

Wengi tulitarajia lile lingekuwa somo juu ya umuhimu kwa serikali kuwa na majenereta ya akiba badala ya kutegemea njia moja tu ya kupata nishati hii muhimu katika Kisiwa cha Unguja.

Miezi mitatu iliyopita likaja pigo kama lile la mwaka 2007, lakini hili likuwa kubwa zaidi na zito na ndiyo maana ilichukua miezi mitatu kwa hali kurudi kama ya kawaida.

Ulipokatika umeme hivi karibuni wengi tuliterejea kuwepo nishati mbadala, ijapokuwa kwa njia ya mgawo kwa vile ilielezwa kwamba serikali, baada ya kupata fundisho la kukatika umeme mwaka 2007, ilikuwa imejipanga vizuri ili hali kama hii isirudie tena.

Wakati ule tuliambiwa serikali ilikuwa mbioni kutafuta majenereta ya akiba na hata kusikika habari za majenereta hayo ya akiba kupatikana, lakini kumbe zile zilikuwa sawa na kile ambacho watu wa jamii ya Wahindu wasiojua vizuri Kiswahili hukieleza kama : ‘Domo jumba ya maneno.’

Hapo tena wale wenye uwezo afadhali wa kiuchumi wakahangaika huku na kule, wakajipiga moyo konde na kununua majenereta ya aina kwa aina, yakiwamo yale ambayo yamepigwa marufuku katika baadhi ya nchi, kwavile si salama au yanatoa moshi mwingi na kuharibu mazingira. Kupata majenereta mabovu hapa kwetu ilionekana kama neema badala ya nakama.

Majenereta haya yalizusha kelele kila pembe ya kisiwa, hasa mjini, huku moshi mzito ukitanda angani na kuharibu mazingira na kuathiri afya za watu, hasa watoto wadogo.

Matumizi ya majenereta yakawa na gharama kubwa si za kifedha tu, bali pia maisha na masikini ndiye akaumia zaidi na kuelekea kwenye ufukara kutokana na ugumu wa hali ya maisha kwa bei za bidhaa kupanda wakati kipato kimeporomoka.

Wapo watu walioiaga dunia kwa kuvuta hewa ya sumu iliyotokana na moshi mzito wa majenereta ambayo yaliwekwa ndani ya nyumba kwa kujilinda na vibaka ambao walikuwa wakiiba yale yaliyowekwa nje ya nyumba au uwani. Wengine walilipukiwa na kuungua wakati wakiyawasha au kuyazima majenereta.

Matumizi ya vibatari, kandili, karabai na mishumaa nayo pia yalileta hasara na maafa mbali mbali.

Watu wnegi walikosa ajira, hasa katika sekta ya utalii kutokana na baadhi ya hoteli kubwa kufungwa kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na kupungua sana kwa wageni waliofika Zanzibar wakati ilipokuwa katika kiza. Wengine walioathirika ni pamoja na mafundi wa vitu vya umeme, maseremala, mafundi cherehani, wafanyabiashara za juisi na kina dada wanaosuka na kutengeneza nywele katika saluni.

Sasa umeme umerudi na kupokewa kwa shangwe na hoi hoi kama wanavyofanyiwa maharusi, japokuwa sehemu nyengine bado hazijapata umeme.

Taarifa ya serikali ilieleza kuwa serikali inaendelea na juhudi za kuleta majenereta yenye uwezo wa kuzalisha megawati 25 ili yatumike kwa dharura. Kwa hivi sasa Zanzibar hutumia umeme wa wastani wa megawati 50 pale kiwango cha matumizi kinapokuwa juu sana kati ya saa 1 na saa 4 usiku.

Tunatarajia juhudi hizi za kupatikana umeme wa akiba ni za kweli na si kama zile kauli za “ tupo mbioni” na hakuna kinachofanywa kama ilivyojitokeza miezi mitatu iliopita baada ya umeme kukatika.

Lakini lilio muhimu si kuja kwa hayo majenereta ya akiba, bali kuhakikisha si mitumba ambayo muda wake wa matumizi unakata roho na yanatunzwa na kuaangaliwa mara kwa mara ili kuweza kufanya kazi vizuri yatakapohitajika kufanya hivyo.

Isije tena yakasahaulika kwa vile umeme kutoka Bara unapopatikana bila ya shida na kutoshughulikiwa na siku umeme utapokatika ndipo pakasikika habari za kuwa yamegundulika kuwa na hitilafu za kiufundi, au hayakuwa na mafuta ya kutosha kuweza kutoa huduma kwa haraka.

Kwa mwananchi wa kawida, kukosekana umeme kwa miezi mitatu kunapswa kutoa fundisho juu ya njia nzuri na salama za matumizi ya majenereta, karabai na mishuma.

Tumeshuhudia majenereta yakiwekwa pembezoni mwa jiko la kuchomea mishikaki au lenye dele la kahawa na galoni za petroli zikijazwa ndani ya gari za abiria. Wengine walikuwa wakiyawasha majenereta huku wakiwa wanavuta sigara. Kwa kweli ilikuwa ni hatari tupu.

Idara ya Zimamoto inapaswa nayo kuwa na utaratibu wa kukagua namna ambavyo majenereta yamefungwa, hasa katika vituo vya mafuta na kama zipo chupa za akiba za kuzima moto na je, wafanyakazi wa hapo vituoni wanajua kuzitumia?

Ni lazima sote tujifunze na tusingojee janga au balaa nyingine kutokea na ndio tukaanza kufikiri nini tufanye. Kiza cha miezi mitatu kilichokikumba kisiwa cha Unguja kinapaswa kutoa mwanga wa kujirekebisha ili balaa kama hili lisitokee tena na libaki katika kumbukumbu za historia ya Zanzibar na kutoa mafunzo ya athari zinazopatikana pale mtu anapokataa kuchukua tahadhari kwa jambo linalohusu maisha yake na ya wenzake.


***Salim Said Salim

.

No comments:

Post a Comment