Thursday, March 25, 2010

SERA YA MAKAAZI YA ISRAEL YAZIDI KUPINGWA

Mpango wa kutafuta amani mashariki ya kati sasa umewekwa njia panda kutokana na tangazo la Israel la kupanua makazi ya walowezi katika eneo la Mashariki ya Jerusalem, huku viongozi wa magharibi wakitakiwa kuchukua hatua.

Akionya juu ya hatua hiyo ya Israel Mfalme wa Jordan Abdullah wa pili ametahadharisha kuwa mpango huo wa kutafuta amani uko njia panda kwa sababu watu wamechoshwa na mchakato usiokwisha katika kupatikana kwa amani katika eneo hilo, hali ambayo haipelekei matokeo yoyote

Katika mahojiano yake na Wahariri wa vyombo vya habari mjini Amman, Mfalme Abdullah amesema anafikiri kuwa dunia nzima inakabiliwa na ukweli kwamba,
tunapigania hatua za kweli, hatua wazi na za haraka kuutatua mzozo huu kwa ufumbuzi wa mataifa mawili, ama kuingia katika mzozo mpya na machafuko ambayo yataathiri ulimwengu mzima.

Kwa upande wake msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran Ramin Mehmanparast amesisitizia umuhimu wa nchi za magharibi kuichukulia hatua Israel na kuongeza kuwa hatua itakazochukua zisiwe tena za maneno bali ziwe za vitendo.

Ameyakosoa vikali pia matamshi yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba matakwa ya kutaka ujenzi huo wa makaazi usitishwe hayana msingi na kwamba Jerusalem siyo makaazi ila ni mji mkuu wao.

Viongozi mbalimbali wa nchi za magharibi ikiwemo Ujerumani tayari wametoa kauli kuhusiana na tangazo lake hilo la kupanua makaazi.


Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton alisema kuendelea kwa ujenzi huo kunahatarisha kupatikana kwa amani katika eneo hilo

Amesema ujenzi mpya katika Jerusalem ama ukingo wa magharibi unahujumu hali ya kuaminiana ya pande mbili na kuhatarisha mazungumzo yaliyokaribu ambayo ni hatua ya kwanza kuelekea mapatano kamili ambayo pande zote mbili zinasema zinayataka na kuyahitaji.

Kwa upande mwingine, Msemaji wa Mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Ghassan Khatib
akielezea kitendo hicho cha Israel kutetea ujenzi huo, amesema ni uvunjaji wa sheria za kimataifa na kwamba matamshi ya hivi karibuni ya waziri Mkuu
Netanyahu ambayo yanaahidi kuendelea na ujenzi haramu wa makaazi ya walowezi katikia Jerusalem ya mashariki ni ya kusikitisha.

Serikali ya Israel jana ilitoa ruhusa ya ujenzi wa nyumba mpya 20 mashariki mwa Jerusalem.

Tangazo hilo limekuja katika siku ambayo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwa amekutana na Rais Barack Obama wa Marekani mjini Washngton, ikiwa uhusiano wa nchi hizo mbili umetikiswa vibaya na sera hiyo ya makaazi ya Israel.
.

No comments:

Post a Comment