Sunday, March 7, 2010

WAZANZIBARI WAPEWE HAKI YA KUPIGA KURA

Salim Said Salim:

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeanzisha zoezi unaloweza kusema halina kichwa wala miguu na mantiki ya kuwepo kwake haionekani.

Hili ni zoezi la kuorodhesha watu wenye shahada za zamani za kupiga kura, lakini hawajapata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambavyo ndiyo kigezo cha mtu kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura.

ZEC imewataka watu waliokosa vitambulisho kujiandikisha majina yao katika maeneno mbali mbali ya kila wilaya ya Unguja na Pemba ambapo zoezi hili litafanyika. Tangazo la kufanyika zoezi hili linatolewa sambamba na matangazo ya mara kwa mara kwenye gazeti la serikali la Zanzibar Leo, radio na televisheni.

Matangazo hayo yanawahimiza vijana na wanawake wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili wawe na sifa za kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu. Pamoja na kuchagua na kuchaguliwa ni haki ya kila raia hapa visiwani Zanzibr, bado haki hiyo imekuwa ikitolewa kwa hila na mbinde na watawala.

Hiki ni kichekesho kingine cha ZEC ambayo inafikiri ujanja na hadaa zitasaidia katika uendeshaji wa shughuli zao za kutaka kuvuruga uchaguzi.

Tume inaelewa kwamba vipo vikwazo vingi ambavyo vinataka ustadi mkubwa kuviruka ndio Mzanzibari, hasa Mpemba, aweze kuitia mkononi shahada inayokuruhusu kupiga kura. Kama unataka kusema kweli mwenendo huu wa ZEC hauna lengo lolote lile isipokuwa kuuhadaa ulimwengu kwamba tume inawahamsisha watu kujiandikisha kupiga kura na inachukua hatua kuhakikisha watu wanapata fursa ya kuchagua na kuchaguliwa. Lakini kinachofanyika ni kinyume chake.

Nimesema zoezi hili halina mantiki kwa sababu kinachoonekana ni kutaka kuendelea kusumbua na kuwahangaisha watu wanaolilia haki ya kupiga kura. Watu wengi wamehangaika kwa miezi kadhaa katika ofisi za masheha, wakuu wa wilaya na mikoa kuomba vitambulisho na kupatiwa haki ya kupiga kura.

Walichoambulia kwa masheha ni maneno yasiyo chembe ya utekelezaji, wanaambiwa wavute subira kwani hiyo pekee ndiyo yenye kuleta heri. Kinachosikitisha ni kwamba baadhi ya watu waliopewa vitambulisho vya ukaazi ili waweze kupiga kura si wazaliwa wa Zanzibar na wengine wana muda mfupi tangu waiingie katika visiwa hivi. Sijui vigezo vinavyotumika na labda ndiyo maana ZEC haitaki kuliweka wazi daftari la wapiga kura.

Inashangaza kusikia kuwa watu waliohangaishwa kwa miezi wanatakiwa wapoteze tena muda wa kwenda kuorodhesha majina yao baada ya kukosa vitambulisho vya Mzanzibari.

Kama kweli ipo nia safi ya kuwatendea haki watu hawa kwa kuwapa haki yao ya kupiga kura, basi tume ingeliwapatia hati zao za kupiga kura moja kwa moja baada ya kuwaorodhesha na kuthibtisha kuwa na shahada halali za kupiga kura uchaguzi wa mwaka 2005 badala ya kuendelea kuwasumbua.

Ukweli ni kwamba maelfu ya watu wamechoka kusumbuliwa kutafuta hivi vitambulisho ambavyo utoaji wake umejaa mizengwe na uhuni. Tukumbuke watu hawa hivi sasa wanakabiliwa na shida kubwa ya kusaka maji, hasa baada ya kukosekana kwa umeme kwa karibu miezi mitatu sasa.

Mchakato huu uliotangazwa na ZEC unazidi kuwatia unyonge Wazanzibari ambao kwao kila kukicha shida zinazidi kushamiri siku hadi siku huku uchaguzi mkuu nao ukionekana kuzingirwa na mizengwe.

Baadhi yao unapokutana nao hukuuliza uchaguzi ujao ni wa watu wa Visiwani au mamluki watakaoletwa kutoka Bara? Nani anawaleta Visiwnai wapiga kura mamluki ni kitendawili, lakini kama ni mtambuzi hilo halikupi tabu. Kwa namna nilivyoona kwa muda mrefu sasa matukio mbali mbali tangu lilipoanza zoezi la uandikishaji wapiga kura na ninavyoona harakati za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu zinavyoendeshwa na tume ambayo inafanya shughuli zake kwa usiri mkubwa, Idara ya Vitambulisho ambayo imeonyesha ustadi mkubwa wa kutoa takwimu zenye kutia shaka.

Masheha, zaidi ya theluthi mbili ni wastaafu wa Jeshi, Polisi na KMKM, wameweka ujeuri na kiburi mbele na hawajali sheria wala katiba. Wakuu wa wilaya na mikoa nao wanaweka vikwazo vya aina yake na bado nina shaka kama ZEC, ina nia ya kweli na ubavu wa kuufanya uchaguzi ujao wa kuwa huru na wa haki.

Baadhi ya watu hujiuliza ni nani hasa anayeendesha uchaguzi wa Zanzibar? Je ni ZEC, Idara ya Vitambulisho, Ofisi ya Waziri Kiongozi, wakuu wa mikoa, wilaya, masheha au maofisa wa vikosi vva ulinzi vya Muungano na SMZ?

Kinachoonekana ni vurugu na unaweza kusema hakuna uchaguzi Zanzibar, bali kinachotayarishwa ni uchafuzi kama ilivyotokea katika chaguzi zilizopita ambapo watu waliojiandikisha mara tatu, nne na zaidi kuwa wapiga kura hawakushitakiwa kwa sababu walitumikia ‘maslahi ya umma’ .Hawa ndio wale wanaoitwa ‘wenzetu’ na walifanya hivyo kwa mujibu wa ‘utaratibu tuliojiwekea”.

Bado ZEC haijaonyesha kwa vitendo kuheshimu katiba ya nchi na haki za raia, pamoja na kuonyesha utiifu kwa kauli aliyoitoa zaidi ya mara tatu Rais Amani Abeid Karume karibuni ya kutaka kila mwenye haki ya kupiga kura apewe haki hiyo bila ya pingamizi au usumbufu.

Watanzania na hasa wa Visiwani wanapaswa kujiuliza kwa nini katika nchi nyingine na hata Bara si shida kwa mwananchi kupata haki ya kupiga kura na iwe balaa kwa Zanzibar?

Ninarudia kusema, kwa kinywa kipana, kuwa kama Zanzibar inataka kujiepusha na vurugu kama zilizoonekana katika chaguzi ziliopita za mfumo wa vyama vingi vya siasa basi ubaguzi katika utoaji wa shahada za kupiga kura ukomeshwe na vitisho katika vituo vya kupiga kura na katika nyumba za watu visiwepo.

Zipo habari kuwa hivi sasa vikundi vya vijana wanaoitwa Janjaweed ambao walifanya fujo za aina yake katika uchaguzi wa mwaka 2005 na kusababisha watu kuuawa na wengi kuwa vilema vinaimarishwa.

Vijana hawa wanasemekana kufunguliwa kambi sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba na wanaonekana asubuhi wakifanya mazoezi barabarani na katika fukwe za bahari.

Hali hii haitoi sura nzuri na inatia shaka kama ipo nia ya dhati ya kuwa na uchaguzi huru, wa haki na amani Visiwani. Wazanzibari ambao sasa wameonekana kuelewana na wote kutaka kumaliza siasa za chuki na uhasama wanapaswa kuonyesha nia hiyo ya kusema yaliyopita yamepita na tugange yajayo kwa vitendo na si kwa kauli peke yake.

Ni muhimu kwa kila Mzanzibari, iwe katika chama tawala cha CCM au kambi ya upinzani, kujifunza kutokana na makosa yaliyofanyika siku za nyuma na kuhakikisha hayarudiwi. Kujaribu kuyarudia makosa wakati tunaelekea uchaguzi mkuu halitakuwa kosa, bali itakuwa ni kutenda dhambi.

Nafasi iliyopatikana karibuni ya kuwepo maelewano baada ya mkutano wa Rais Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, inapaswa kutumika vizuri.

Ikipotea itakuwa si rahisi kuipata tena siku za mbele. Sote tujifunze kutokana na makosa tuliyoyatenda au waliyoyafanya wenzetu ndani na nje kiasi cha chaguzi kuleta balaa badala ya manufaa.

No comments:

Post a Comment