Friday, March 19, 2010

PANDE NNE ZASIKITISHWA NA HALI YA GAZA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameitaka Israel kusitisha shughuli zote za ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Waarabu.

Akizungumza katika mkutano wa pande nne zinazotafuta amani ya Mashariki ya Kati, huko Moscow, Urusi, katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia ameelezea kusikitishwa kwake na hali ilivyo katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Viongozi katika mkutano huo wa mjini Moscow pia wamesema wanataka kuona Israel na Palestina zinarejea katika meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo.

Pande hizo nne, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani na Urusi, zinakutana mnamo wakati ambapo hali katika eneo la mashariki ya kati inaendelea kuwa tete.

Hatua ya Israel kutangaza ujenzi wa nyumba mpya 1600 za walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Waarabu ya Jerusalem Mashariki, imeshutumiwa na jumuiya ya kimataifa kuwa inazikwaza juhudi za kufufuliwa kwa mazungumzo kati ya Israel na Palestina.

Mkuu wa sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, jana alikuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kutoka Umoja wa Ulaya kuzuru Ukanda wa Gaza, ambako aliitaka Israel kuruhusu kuingia misaada huko Gaza ili kusaidia ukuaji wa uchumi.

Kwa upande mwengine, Ndege za Israel zimeshambulia Gaza, baada ya mtu mmoja kuuawa hapo jana nchini Israel, kufuatia kombora lililorushwa kutokea Ukanda wa Gaza .


.

No comments:

Post a Comment