Monday, March 29, 2010

MIAKA MIWILI BAADA YA MAKUBALIANO MAGEUZI BADO NI NDOTO KENYA

Mwezi Machi 2008, wanasiasa mahasimu nchini Kenya walikuwa wakipiga zumari la mabadiliko ya kisiasa na Jumuiya ya kimataifa ikipongeza mafanikio ya kupatikana suluhisho la mgogoro uliozuka baada ya uchaguzi mwishoni mwa 2007, jambo ambalo ni nadra barani Afrika.

Lakini pamoja na hayo miaka miwili baadae hali halisi iliopo ni tofauti kabisa .
Mwana harakati mmoja anasema ilikuwa ni lazima zifanyike jitihada za kuinusuru Kenya baada ya machafuko na mauaji yaliotokana na uchaguzi mkuu wa Desemba 2007.

Makubaliano yaliosainiwa Februari 28 2008 na kuanza kufanya kazi mwezi Machi mwaka huo, juu ya kugawana madaraka, yalikua na ahadi ya kufanyika marekebisho.

Lakini kuna wanaodai kwamba sambamba na baraza la mawaziri kufanywa kuwa kubwa ili kuzihusisha pande zote zilizohusika katika mgogoro huo, hayo sasa yanaonekana kuandamana pia na kuzidi kwa rushwa serikalini. Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa, Kofi Annan, aliyekua mpatanishi miaka miwili iliopita pamoja na dola zenye nguvu za magharibi zilizosaidia kupatikana makubaliano, wanaendelea kuikumbusha Kenya juu ya ahadi zake na kuonya juu ya ulipizaji kisasi na hofu ya kuzuka upya mivutano ya kikabila.

Mnamo takriban ziara yake ya tano nchini Kenya wiki iliopita, Bw Annan alizungumzia kuvunjwa moyo na pia hali ya wasi wasi. Pamoja na kugawana madaraka, lakini utendaji wa serikali ya muungano nchini humo hauridhishi kwa sababu ya mivutano isiyokwisha na mtu anaweza kusema imeshindwa kuwajibika kama Wakenya walivyotarajia.

Mgogoro wa hivi karibuni tu ni ule uliozuka baada ya waziri mkuu Raila Odinga kutangaza anawasimamisha mawaziri wawili waliotajwa katika kashfa tofauti hadi uchunguzi umekamilika. Hao walikua ni waziri wa kilimo William Ruto na wa elimu Profesa Sam Ongeri.

Lakini hatua hiyo ikapingwa na Rais Kibaki akisema Odinga hana mamlaka hayo na wala hakumshauri. Kibaki akawataka mawaziri hao waendelee na kazi zao. Baadhi ya wadadisi wanasema mivutano katika serikali ya Kenya sio tu jambo linalomvunja moyo.

Bw Annan kama mtu aliyekua mpatanishi , lakini pia mabalozi wa nchi za magharibi waliokua wakisaidia suluhisho lipatikane. Sasa wanaonekana kama nao wameshindwa na sasa wanazungumzia athari zake, pindi wanasiasa wa Kenya hawatakuwa makini.
Afisa mmoja wa kibalozi aliyetaka asitajwe jina amesema kwa mtazamo wa migogoro mengine barani Afrika, tangu ulipozuka ule wa Kenya, kuna umuhimu wa kuzingatia ujumbe uliotolewa kwa watawala katika mgogoro wa kisiasa Zimbabwe au nchini Madagascar.

Anasema la sivyo mtindo wa watawala kufanya mizengwe ukiwemo wizi wa kura wakati wa uchaguzi ili wabakie madarakani utaendelea.

Mwanaharakati Mwalimu Mati anasema Kwa Kenya, inaonekana hata miaka miwili baada kutiwa saini makubaliano ya kugawana madaraka, mivutano iliopo haina dalili ya kumalizika.

Anasema Rais Kibaki hataki kuona yaliokubaliwa yanatekelezwa kwa sababu yatamaliza madaraka makubwa aliyonayo kama rais na Odinga hatoregeza kamba kwa sababu akiwa kama Waziri mkuu anataka atambuliwe kuwa ni mkuu wa serikali nao mawaziri hawatotaka kuona mivutano inamalizika na wanawajibika kwa sababu wanataka waendelee katika nyadhifa zao na kuwepo nafasi zaidi ya uporaji mali ya umma. Mwanaharakati huyo anamaliza kwa kusema hali hii ni sawa na " njama iliopangwa barabara dhidi ya umma wa Kenya."

.

No comments:

Post a Comment